Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo anaongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa ngazi ya Makatibu Wakuu wa Utatu wa Asasi mbili za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) unaofanyika Lusaka, Zambia Machi 22, 2024.
Mkutano huo ni maandalizi ya Mikutano ya ngazi ya Mawaziri na Wakuu wa Nchi na Serikali itakayofanyika tarehe 22 na 23 Machi 2024 mutawalia.
Wakati wa ufunguzi wa Mkutano huo, Mwenyekiti ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ya Zambia, Bi. Etambuyu Anamela Gundersen alisema mwitikio mkubwa wa wajumbe kushiriki mkutano huo ni ishara ya wazi kuwa nchi wanachama zimedhamiria kumaliza changamoto za kiuslama katika kanda ya SADC, hususan Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Jimbo la Cabo Delgado nchini Msumbiji.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) watashiriki Mkutano wa ngazi ya Mawaziri ambao umepangwa kufanyika mchana na utakamilisha agenda zitakazojadiliwa katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Philip Isdor Mpango atamwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkutano huo.