Na Dk. Reubeni Lumbagala, Kongwa, Dodoma.
Imetimia miaka mitatu leo tangu Rais Samia aapishwe kuwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Tanzania ili kuwatumika Watanzania na hatimaye kuendeleza juhudi za kuwaletea maendeleo.
Baada tu ya kuapishwa Machi 19, 2021, Rais Samia ameendelea na jukumu la msingi la kulinda amani na mshikamano wa nchi na kuhakikisha Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020-2025 inatekelezwa kikamilifu ili kuendeleza imani waliyonayo wananchi kwa CCM na serikali yake katika kuwatumikia na kuwaletea maendeleo kama walivyoahidiwa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
Katika kufanikisha mipango na mikakati ya serikali ya kukuza na kuchochea maendeleo ya nchi na watu wake, Tanzania haina budi kujifunza na kushirikiana na nchi nyingine ndani na nje ya bara la Afrika kwani Tanzania si kisiwa, na ndiyo maana suala la diplomasia limepewa msukumo na msisitizo wa kipekee na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi mahiri wa Dk. Samia Suluhu Hassan.
Dunia imebadilika sasa, badala ya masuala ya diplomasia kujielekeza zaidi katika kuimarisha mahusiano kati ya nchi na nchi, sasa mambo yamebadilika. Nchi zinatumia mahusiano yake na nchi nyingine kwa manufaa ya kiuchumi, na hapo ndipo mkazo ulipo kwa nchi nyingi duniani.
Rais Samia ameimarisha sana diplomasia na nchi washirika wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Mathalani, baada ya kupishwa kuwa Rais, safari yake ya kwanza ilikuwa nchini Kenya kwa majirani zetu wa karibu.
Huko Rais alipata fursa ya kuhutubia Bunge la nchi hiyo na kupitia mazungumzo na viongozi wa Kenya, vikwazo 64 vya biashara vilivyokuwepo kati ya Tanzania na Kenya vilitatuliwa.
“Wote ni mashahidi malori yalikuwa yanakaa mwezi mzima mpakani Kenya na Tanzania, vifaranga hadi vikachomwa moto na mahindi yalikaa hadi yakaota sumu kuvu. Lakini nilipokwenda tulizungumza tukaondoa vikwazo vyote 64. Sasa hivi biashara ya Kenya na Tanzania imekua kwa kiwango kikubwa. Tena faida imekuja upande wetu,” anasema Rais Samia.
Si Kenya pekee, bali pia Rais Samia alisafiri kuelekea nchini Uganda kwa ajili ya utiaji saini mikataba ya utekelezaji wa mradi wa bomba la mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani,Tanga (EACOP).
Katika mradi, juzi Jumapili ilielezwa kuwa mradi huo umeanza kuleta faida kupitia kodi mbalimbali zinazofikia takribani shilingi bilioni 30 na kuzalisha ajira kwa Watanzania. Akiongea na vyombo vya habari, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), Deus Sangu alisema kamati imejiridhisha na maendeleo ya mradi ambao unajengwa na kuwa na matarajio makubwa katika kuchangia kwenye uchumi wa Taifa.
Serikali ya Uganda na Tanzania zimekubaliana kujenga Mradi huu wa kimkakati wenye kilomita 1,445 ambapo kwa Tanzania pekee kuna kilometa 1,147. Mpaka kukamilika mradi unatazamiwa kugharimu Dola za Marekani bilioni 5.1 (takribani shilingi trilioni 11).
Katika kuifungua zaidi Tanzania kimataifa ili kuimarisha diplomasia ya kiuchumi na mataifa mengine, Rais Samia amesafiri katika nchi za Burundi, Ethiopia, Namibia, Malawi, Zimbabwe, Afrika Kusini na Rwanda. Katika ziara hizi, Rais Samia ameendelea kushawishi wawekezaji na wafanyabiashara kuja kuwekeza Tanzania kutokana na uwepo wa mazingira mazuri na rafiki kwa ajili ya uwekezaji na biashara.
Rais Samia amefanya juhudi kubwa za kuimarisha uhusiano kati ya Tanzania na Marekani, ambapo katika ziara yake nchini humo alikokwenda kwa dhumumi la uzinduzi wa Filamu ya Royal Tour, alishuhudia utiaji saini wa mikataba yenye thamani ya shilingi trilioni 11.
Aidha, Rais Samia pia ameimarisha diplomasi ya kiuchumi na nchi za Ulaya na Umoja wa Falme za Kiarabu. Mathalani, Rais Samia alipozuru Falme za Kiarabu katika maonesho ya Kimataifa ya Biashara (Dubai Expo 2020), alishiriki utiaji saini wa mikataba ya makubaliano 37 yenye thamani ya Sh trilioni 17. Pia Tanzania imenufaika na msaada wa Sh trilioni 1.17 kutoka Umoja wa Ulaya (EU) ikiwa ni sehemu ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya kukabiliana na janga la Uviko-19.
Rais Samia pia alipata mwaliko wa kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki duniani na nchi ya Vatican, Papa Francis. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Januari Makamba alisema lengo la ziara hiyo ilikuwa ni kukuza ushirikiano kati ya Tanzania na Vatican, ushirkiano ulioanza tangu mwaka 1960.
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje inaonesha Kanisa Katoliki linakadiriwa kumiliki zaidi ya shule za chekechea 240, shule za msingi 147 na shule za sekondari 245, vyuo vya ufundi 110, na vyuo vikuu vitano huku taasisi za afya 473 zikiendeshwa na Kanisa Katoliki.
Katika mazungumzo ya faragha yaliyodumu kwa takribani dakika ishirini na tano, wawili hao waliridhika na uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Vatican, huku Kanisa Katoliki likipongezwa kwa juhudi kubwa katika ustawi, maendeleo katika sekta za elimu, afya na ustawi wa jamii.
Viongozi hao pia walizungumzia masuala ya kijamii, kikanda na kimataifa, ikiwamo umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika kudumisha amani duniani. Baada ya Rais Samia kumaliza ziara ya siku mbili Vatican, Februari 13, 2024 aliwasili jijini Oslo nchini Norway kwa ziara ya kitaifa ambapo alikutana na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Bunge la Norway (Storting) Svein Harberg, na mwenyeji wake Mfalme Harald V na Malkia Sonja.
Katika ziara hiyo, Rais Samia kupitia wajumbe walioshiriki Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Norway lililofanyika jijini Oslo, aliwaalika na kuwakaribisha wawekezaji kutoka Norway kuja kuwekeza nchini kwenye sekta za gesi, mafuta, nishati mbadala, kilimo na mifuko ya uwekezaji na usafirishaji.
Itoshe kusema, ziara hizi za kidiplomasia alizofanya Rais Samia katika nchi mbalimbali, zina manufaa chanya katika ujenzi wa uchumi na maendeleo ya nchi yetu.
Si tu kwamba Rais Samia amesafiri nchi mbalimbali, bali pia viongozi wa nchi nyingi wametembelea Tanzania katika kuimarisha diplomasia ya kiuchumi. Ujio wa viongozi kutoka nchi mbalimbali mara kadhaa umeambatana na wafanyabiashara na wawekezaji wakubwa ambao wamekuja kujionea maeneo ya uwekezaji na biashara ili kuwekeza Tanzania.
Taarifa iliyotolewa na Kituo cha Uwekezaji (TIC) mwanzoni mwa mwaka ikionesha kwamba mwaka jana, 2023 kituo hicho kilisajili miradi 504 yenye thamani ya Dola za Marekani Bilioni 5.6, sawa na takribani shilingi trilioni 10.
Idadi hiyo ni ongezeko la asilimia zaidi ya 100 ikilinganishwa na miradi 132 iliyosajiliwa katika kipindi kama hicho mwaka 2022. Hakika, miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia, diplomasia ya uchumi imeimarika sana na hivyo kusaidia katika kufanikisha mipango mbalimbali ya nchi na hivyo kuharakisha maendeleo ya Watanzania.
Mwandishi ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Mlali iliyoko wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma. Maoni – 0620 800 462.