Mkurugenzi Mkuu wa kituo cha kimataifa cha mikutano Arusha (AICC),Christine Mwakatobe akizungumza na waandishi wa habari mkoani Arusha ,pembeni yake ni Mkurugenzi Mtendaji wa bodi ya utalii Tanzania (TTB),Ephraim Mafuru.
…….
Happy Lazaro,Arusha.
Arusha .Mkuu wa kituo cha kimataifa cha mikutano Arusha (AICC) ,Christine Mwakatobe amesema kuwa atahakikisha mapato yanaongezeka kwa kiasi kikubwa kwa kutumia mbinu mbalimbali ikiwemo kukutana na wateja mmoja mmoja ili kuweza kupata maoni ya wateja na kuweza kuboresha kituo hicho.
Ameyasema hayo leo mkoani Arusha ,wakati wa kikao na waandishi wa habari katika kueleza mikakati mbalimbali ambayo ataanza nayo kuhakikisha kituo hicho kinaendelea kupaa na kuvuka malengo.
Mwakatobe amesema kuwa,atahakikisha mapato yanaongezeka kwa kiwango kikubwa na kuhakikisha lile gawio la serikali kwa mwenye Mali ambaye ni Msajili wa hazina /serikali linaongezeka ili kuchangia miradi ya kimkakati ya serikali.
Ameongeza kuwa,atajikita katika kuongeza vyanzo vipya vya mapato na kuongeza mapato ya shirika,kutekeleza miradi ya maendeleo iliyoainishwa kwa weledi na weledi mkubwa,kuboresha maslahi ya wafanyakazi ambao ndio nguvu kazi ya shirika.
Aidha amesema kuwa, ataongeza kasi ha ushirikiano na wadau muhimu katika sekta ya utalii kama TTB,TANAPA,KADCO /KIA ,Tantrade ,ambapo atahakikisha anaboresha namna ya kuwahudumia wateja kwa maana ya kutoa huduma inayokidhi matarajio ya wateja.
“Pamoja na mikakati mbalimbali ambayo nimejipanga kuanza nayo nitaendelea kutangaza ukumbi wa mikutano wa AICC na ule wa Dar kuhakikisha unajulikana duniani kote.”amesema.
Amesema kuwa ,kituo.hicho kimekuwa kikishiriki katika utalii wa mikutano na wataendelea kutangaza filamu ya Royal Tour huku wakihakikisha mipango uliyowekwa inaendelea kutekelezwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa bodi ya utalii Tanzania (TTB) ,ambaye alikuwa Mkurugenzi mkuu wa AICC ,Ephraim Mafuru amesema kuwa,wakati akiwa katika nafasi hiyo amejitahidi kufufua miradi iliyokuwa imekufa kwa zaidi ya miaka 16 iliyopita ambapo mikakati zaidi aliyokuwa amejiwekea ni kujenga hoteli ya nyota tano na kumbi zingine huku michoro ikiwa imeshaanza.
“Mikakati yote niliyokuwa nimeweka na kuianza itaendelea kutekelezwa tukishirikiana kwa pamoja lengo likiwa ni kufikia malengo yaliyowekwa “amesema.