KATIKA Kutekeleza Sheria ya Madini ya mwaka 2010 na marekebisho yake ya 2017 inayozuia madini ghafi kusafirishwa nje ya nchi, Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) kimejipanga kuhakikisha Sekta ya Madini inaendelea kuimarika kwa uongezaji thamani madini nchini kuendelea kuleta faida zaidi
Hayo yamebainishwa leo Machi 21, 2024 na Kaimu Mratibu wa Kituo hicho Ally Maganga akizungumza na waandishi wa habari waliopo katika zaira ya kutembelea miradi ya Kituo hicho kilichopo jijini Arusha.
Maganga ameongeza kuwa ili kufanikisha hilo, wamekuwa wakitoa mafunzo ya uongezaji thamani madini, kwamba madini yaliyoongezwa thamani yanafaida kubwa ikilinganishwa na Madini ghafi.
Maganga amebainisha kuwa lengo la Sheria hiyo ni kuhamasisha ujenzi na uanzishaji wa viwanda vya uongezaji thamni madini jambo ambalo TGC imejipanga kutekeleza ili kuongeza fursa za ajira kwa vijana pamoja kuleta fedha za kigeni nchini.
“Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na marekebisho yake ya Mwaka 2017 hairuhusu kusafirisha Madini ghafi nje ya nchi, hii ni kwasababu yanakwenda kutengeneza ajira nje, lakini kwa upande mwingine Sheria hii inachochea ajira nchini kwani kuna vijana wanapata ajira hapa kwenye Kituo chetu na nje ya kituo kwa kuongeza thamani madini na wengine wanapata kwenye viwanda ambavyo vinafanya uthaminishaji madini,” amesema Maganga.
Maganga amefafanua kwamba TGC ina mpango wa kuwapeleka vijana kupata utaalam na uzoefu katika tasnia ya uongezaji thamani Madini kwenye nchi ambazo tunaushirikiano nazo ikiwemo Thailand.
Kwamba lengo ni kupata wataalam wengi ambao watakuwa na manufaa kwa Taifa, lakini pia TGC inampango wa kuwaunganisha vijana nje ya nchi ambao wana utaalam huo katika mataifa ambayo yanauhitaji.
Awali Mganga ameeleza kuwa Kituo kimeweka mikakati ambayo itakuwa chachu ya mageuzi makubwa kwenye Sekta ya Madini hususan katika uongezaji wa thamani ya madini ya vito nchini.
Ameitaja mikakati hiyo ni pamoja na ujenzi wa jengo la kisasa litakalo kuwa na ghorofa nane (8), kutanua wigo wa kutoa huduma za maabara, kuanzisha makumbusho ya madini ya vito na mkakati wa utafiti wa masuala ya Madini ya Vito hapa nchini.
Kwa upande wa kutanua wigo wa kutoa huduma za maabara, amesema lengo ni kusaidia watu wajue thamani halisi ya bidhaa zitokanazo na madini ya vito ikiwemo Pete, Vidani , kupitia maabara ambazo zitawekwa maeneo yote yenye shughuli za uchimbaji wa Vito.
Hata hivyo Maganga amezungumzia kuhusu mkakati wa Utafiti wa masuala ya Madini ya Vito hapa nchini, amesema itasaidia katika usanifu wa masuala mbalimbali yanayohusu Madini hayo, hivyo watafanya maboresho katika eneo la utafiti jambo ambalo litasaidia katika kupata taarifa sahihi za Madini na kujua namna nzuri ya kuyatunza kwa ubora na thamani kubwa.