*Eneo la Tajiri- Handeni lina tani milioni 268 za mashapo ya Madini Tembo ikijumuisha tani milioni 74 za mashapo yaliyothibitika
*Mgodi kuingizia Serikali Mapato dola za Marekani milioni 437.96 (Trilioni 1.12 Tshs) kutokana na gawio la hisa za Serikali, kodi na tozo
*Kiwanda kuchakata na kuzalisha metali zenye ubora
Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde amesema kuwa Tanzania imeandika historia kwa kuwa na mgodi mkubwa wa uzalishaji wa Madini Tembo na kiwanda kikubwa cha Usafishaji wa Madini ya Metali-Anuai, Miradi itakayochochea Ukuaji na Mchango wa Sekta ya Madini katika Pato la Taifa na maendeleo ya kiuchumi nchini.
Amesema hayo leo Machi 21, 2024 Jijini Dodoma wakati akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya Leseni ya Uchimbaji Mkubwa Madini Tembo (Heavy Mineral Sands) kwa Kampuni ya Nyati Mineral Sands Limited na leseni ya Kiwanda cha Uchenjuaji wa Madini ya Metali kwa Kampuni ya Tembo Nickel Refining Company Limited.
Akizungumzia Mradi wa Uchimbaji Mkubwa wa Madini Tembo, Waziri Mavunde amesema, Katika shughuli ya Utafiti wa Madini iliyofanywa na kampuni tanzu ya Jacana Resources ilibaini kuwa eneo la Tajiri lilopo Wilaya ya Handeni mkoani Tanga lina kiasi cha takribani tani milioni 268 za mashapo ya madini ya heavy mineral sand ikijumuisha tani milioni 74 za mashapo yaliyothibitika.
Kuhusu Kiwanda cha kuchakata Madini ya Metali-Anuai cha Tembo Nickel Refining Limited kitakachojengwa Kahama mkoani Shinyanga, Mhe. Mavunde amesema, Ujenzi wake utakuwa ni utatuzi wa changamoto iliyokuwepo kwa Wachimbaji wa Madini ya metali nchini kulazimika kusafirisha makinikia ya metali kwenda kwenye viwanda vya nje ya nchi kwa ajili ya uchenjuaji ili kupata zao la mwisho au kuuza madini katika hali ya makinikia kwa bei ya chini.
“Kwa kupitia teknolojia hiyo makinikia yatakayozalishwa katika mgodi wa Kabanga na mingine nchini yataweza kuchakatwa na kuzalisha metali zenye ubora.” amesisitiza Mavunde.
Vilevile, Mhe. Mavunde ametoa wito kwa Wachimbaji na Wamiliki wa Migodi inayozalisha makinikia nchini kutumia kiwanda hicho kuchakata madini hayo pindi kitakapo kamilika ili kukuza fursa za ajira na mapato yatokanayo na rasilimali madini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Nyati Mineral Sands Limited, Jozsef Patarica amesema kwamba Mradi huo utaleta manufaa makubwa kwa Tanzania kwani utasaidia kuongeza maarifa, kutengeneza ajira lakini pia kuchangia mapato ya Serikali kupitia kodi mbalimbali.
Kampuni ya Nyati Mineral Sands Limited ni Kampuni ya ubia baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yenye umiliki wa hisa asilimia 16 na Kampuni ya Strandline Resources Limited ya Australia yenye umiliki wa asilimia 84 ambapo Serikali inatarajiwa kukusanya mapato takribani dola za Marekani milioni 437.96 (Trilioni 1.12 Tshs) kutokana na gawio la hisa za Serikali, kodi na tozo mbalimbali; kupatikana kwa fursa za ajira za moja kwa moja zipatazo 150 ikijumuisha ajira 140 za watanzania na 10 za wageni.
Naye, Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Lifezone Metals kwa niaba ya Kampuni ya Tembo Nickel, Chris Showalter amesema kuwa Kiwanda hicho cha Uchenjuaji cha Kahama ni kielelezo cha mafanikio ya Tanzania na kwamba hatua hiyo ni kuandaa jukwaa pana litakalobeba kitovu cha uchimbaji, uchakataji na uchenjuaji wa madini ndani ya Ukanda Maalum wa Kiuchumi wa Buzwagi wilayani Kahama mkoani Shinyanga
“Tutachimba, tutachakata, tutachenjua Madini ya Kimkakati hapa hapa nchini” amesisitiza Showalter.
Kiwanda cha Usafishaji wa Madini kitamilikiwa na Kampuni ya Tembo Nickel Refining Limited ambayo ni Kampuni tanzu ya kampuni ya ubia ya Tembo Nickel Corporation Limited ambayo inamilikiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Kampuni ya Lifezone Metals ya Uingereza iliyosajiliwa katika soko la hisa la marekani (NYSE:LZM).
Matukio hayo mawili yamekwenda sambamba na tukio la uhuishaji wa Leseni ya Uchimbaji Madini ya Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu uliopo Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga unaomilikiwa na Kampuni ya Barrick Gold Mine.