Na. Damian Kunambi, Njombe
Ili kuhakikisha uzalishaji wa zao la Kahawa unaongezeka kutoka 218gm hadi 500gm kwa mti mmoja Wilayani Ludewa mkoani Njombe Mkuu wa wilaya ya Ludewa Victoria Mwanziva akiwa sambamba na Mkurugenzi wa halmashauri ya Wilayani hiyo pamoja na Wataalam wa Idara ya Kilimo wametembelea Kiwanda cha City Coffee kilichopo jijini Mbeya na kufanya kikao kazi kilicholenga kuongeza tija katika uzalishaji huo wa Kahawa.
Bi. Mwanziva amesema kuwa Sanjari na kikao kazi hicho lakini pia walitembelea shamba la Kahawa la Utengule mkoani humo kwa lengo la kujifunza teknolojia ya kisasa ya uzalishaji Kahawa na uzalishaji wa miche bora ili kufikia lengo la uzalishaji miche 290,000 ifikapo mwaka 2024/2025 kwani kwa sasa wanazalisha miche 188,480 pekee.
“Wilaya ya Ludewa kwa Mwaka 2023/2024 imezalisha Jumla ya Tani 150 za Kahawa na sasa inakwenda kwenye mkakati makhsusi wa kuzidi kuongeza tija kwenye uzalishaji wa zao hili la kimkakati kwani Kahawa ni zao la biashara ambalo lenye uwezo wa kuinua Uchumi wa Mkulima, Wilaya na Taifa hivyo Ludewa tuna hekta 21,300 ya eneo linafaa kwa kilimo hiki na tutaenda kulitumia vyema kwa kilimo hiki cha kahawa” . Amesema Bi. Mwanziva.
Ameongeza kuwa tayari Mikakati mbalimbali imewekwa ya kuhakikisha uzalishaji huo wenye tija unafanikiwa ikiwemo Kutoa Mafunzo zaidi kwa Wakulima, Maafisa Ugani na vyama vya Ushirika, kuongeza ubora wa Kahawa, Kuongeza tija kwenye Uzalishaji, Kuongeza teknolojia pamoja na uzalishaji miche bora ya Kahawa.
Aidha kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Sunday Deogratius amesema wanampango wa Kufufua kahawa ya zamani kwa kuanza na Ha 5.8 (sawa mibuni 7,800) ambapo mwaka 2023/2024 itafufuliwa na kuwahimiza wakulima kuitunza mibuni hiyo sambamba na Kuhamasisha wakulima wanapovuna kahawa mbivu kuipeleka kwenye mtambo wa kukoboa (CPU) ili kupata kahawa iliyo bora na yenye thamani kubwa sokoni.
” Halmashauri yetu ina vyama vya ushirika vya wakulima wa zao la kahawa viwili ambavyo ni Ludewa Coffee Growers na Mawengi Coffee Growers vyama hivi tayari vina miliki mashine zao za kumenyea kahawa (CPU’s) hivyo tunahitaji wakulima wote kutumia mashine hizi ili kupata kahawa iliyo bora zaidi”, Amesema Deogratius.
Sanjali na hilo Mkurugenzi huyo amesema kumekuwa na baadhi ya wafugaji wa Ng’ombe wa Halmashauri hiyo kuacha mifugo yao milimani huku ikijichunga yenyewe hivyo halmashauri hiyo imeazimia kuhakikisha mifugo hiyo inayoachwa huria milimani inarudishwa mazizini na kufugwa kitaalam ili kupata samadi ambayo itatumika katika mashamba ya kahawa.