Na WMJJWM, Dar Es Salaam
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ametoa wito kwa viongozi kuhakikisha udhibiti wa wimbi la watoto wanaokimbilia kuishi na kufanya kazi mitaani unaenda sambamba na kuimarisha Kamati za Ulinzi wa Watoto na Wanawake katika mamlaka za Serikali za mitaa.
Waziri Dkt. Gwajima ametoa wito huo Machi 20, 2024 kwa nyakati tofauti wakati wa ziara yake wilaya za Kigamboni na Ilala mkoani Dar Es Salaam kwa lengo la kufuatilia jinsi gani mkoa unadhibiti wimbi la watoto waishio na kufanya kazi mitaani.
Amebainisha kwamba, kwa mujibu wa Mpango kazi wa Taifa wa kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) kamati hizo zipo katika
ngazi za kijiji, mitaa na kata ambapo, viongozi wa Serikali ngazi husika ndiyo wenyeviti na makatibu ni walimu au wataalamu wa kisekta.
Amesema pia, kundi kubwa la watoto hao lilipaswa kuwa shuleni lakini kutokana na changamoto mbalimbali zikiwemo kulegalega kwa kamati hizo zenye wajumbe wa kisekta, utoro wa watoto hao shuleni hukosa ufuatiliaji hadi ngazi ya kaya hivyo hukimbilia mitaani.
“Naombeni viongozi muhakikishe kamati za ulinzi wa wanawake na watoto zinapata idadi ya watoto waliotoroka shuleni sambamba na kubaini kaya wanazotoka ili kufanya uchambuzi wa mazingira ya kaya hizo na kuchukua hatua za maendeleo na ustawi wa jamii ili watoto hao wanaporejeshwa nyumbani wasitoroke tena. Uchambuzi wa hali ya maendeleo na ustawi wa jamii kwa kila kaya vema ikajulikana mapema na hatua kuchukuliwa ili kuepuka watoto hao kukimbia familia zao na kwenda mtaani kwani ni bora zaidi kuzuia mtoto asifike mtaani” amesema Waziri Dkt Gwajima.
Aidha amesisitiza, Maafisa Maendeleo ya Jamii na Maafisa Ustawi wa Jamii wakishirikiana na Wadau wa maendeleo kusaidia kuchambua na kushauri juu ya ufumbuzi wa changamoto za kimaendeleo na kiustawi kwenye kila kaya wanakotokea watoto wanaoonekana kuwa na changamoto ili kudhibiti kabla watoto hao hawajakimbia shuleni na kwenye familia.
“Pale tu ambapo kamati za ulinzi wa watoto ngazi ya Serikali za mtaa zenye wajumbe wa kisekta zitakaposimama na kufanya majukumu yake kwa wakati na kwa ufanisi ndipo tutakapoweza kubaini kaya zenye changamoto ambazo zinaweza kuchangia watoto kuacha shule na kukimbilia mitaani na kuchukua hatua stahiki kabla watoto hao hawajatoweka, hivyo vema waheshimiwa wakuu wa mikoa na wilaya wafahamu mifumo hii na wasimamie ifanye kazi” amesisitiza Waziri Dkt Gwajima.
Kwa upande wao Wakuu wa wilaya za Kigamboni Mhe. Halima Bulembo na Ilala Mhe. Edward Mpogolo wamemshukuru Waziri Dkt. Gwajima kwa ziara hiyo iliyotoa elimu na kuhamasisha kuendelea kupambana na changamoto hiyo, ambayo imeendelea kufanyiwa kazi na kuwekewa mikakati bado kuna kazi kubwa ya kufanya.
Katika ziara hiyo, Mhe. Waziri Gwajima ametembelea shule ya msingi Maweni, Kigamboni na shule ya msingi Mchikichini, Ilala pamoja na baadhi ya familia zenye changamoto.