Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Mheshimiwa Stansalaus Mabula akiangalia mchoro wa ramani ya Jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Tarime wakati Kamati ilipotembelea na kukagua mradi huo.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Mheshimiwa Stansalaus Mabula akiangalia daftari la mmoja wa wanafunzi kutoka shule mpya ya sekondari iliyopo Kijiji cha Nyasaricho katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime wakati Kamati hiyo ilipotembelea na kukagua mradi huo.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Mheshimiwa Stansalaus Mabula akiambatana na wajumbe wa Kamati wakiangalia sehemu ya kunawia mikono nje ya bwalo la kulia chakula wakati kamati hiyovilipotembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa shule mpya ya sekondari iliyopo Kijiji cha Nyasaricho katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.
……..
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), imeutaka uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kutomlipa mkandarasi aliyejenga Jengo la Halmashauri hiyo hadi pale ataparekebisha mapungufu yote katika jengo hilo.
Kauli hiyo ilitolewa na Makamu Mweyekiti wa Kamati hiyo Mheshimiwa Stansalaus Mabula wakati Kamati ilipotembelea na kukagua mradi huo pamoja na mradi wa ujenzi wa shule mpya ya sekondari iliyopo Kijiji cha Nyasaricho iliyopo katika Halmashauri hiyo.
Alisema lazima Mhandisi wa Halmashauri ajiridhishe kwamba kazi iliyofanyika ina ubora unaoridhisha ndipo aweze kulipwa.
“Ni marufuku kumlipa kiasi chochote Mkandarasi ikiwa bado hajakamilisha kazi kwa kiasi kinachotakiwa, Mhandisi ajiridhishe kwamba kazi iliyofanyika imefanyika kwa ustadi na ubora mkubwa,” alisema.
Kamati iliainisha baadhi ya mapungufu katika jengo hilo kuwa nipamoja na umaliziaji (finishing) mbaya na uchafu katika maeneo mbalimbali.
Kwa upande wa shule ya Sekondari, Kamati ilipongeza kwa kazi nzuri iliyofanyika na kuagiza marekebisho madogomadogo ikiwemo kupanda miti ya kutosha.
Aidha, ilitaka kuona taarifa ya ujenzi wa shule hiyo na kuanisha maeneo ambayo yamesababisha gharama za ujenzi kuongezeka.
Kamati ya LAAC kesho tarehe 22 Machi, 2024 itakagua mradi wa ujenzi wa soko kuu la kisasa na ujenzi wa jengo la utawala katika Halmashauri ya Mji wa Tarime.