Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Hajati Fatma Mwasa akizungumza na wananchi waliofika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Bukoba (BRRH) kwa ajili ya kupata huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa BRRH wakati wa ufunguzi wa kambi maalumu ya siku tano ya uchunguzi na matibabu ya moyo ambapo hadi sasa watu 288 wameshapata huduma za matibabu.
……………………..
RC Mwasa: Kagera changamkieni fursa ya kupima moyo
Wananchi wa Mkoa wa Kagera wamehimizwa kufika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Bukoba (BRRH) kwa ajili ya kupimwa na kutibiwa magonjwa ya moyo kutokana na uwepo wa kambi maalumu ya matibabu inayoendeshwa na madaktari bingwa wa magojwa ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).
Rai hiyo imetolewa leo na mkuu wa mkoa huo Mhe. Hajati Fatma Mwasa wakati akifungua kambi hiyo ya kibingwa ya simu tano amabapo wananchi wanapata huduma za kibingwa ikiwa ni pamoja na kipimo cha kuangalia moyo unavyofanya kazi, kipimo cha kuangalia mfumo wa umeme wa moyo, elimu ya lishe bora na matumizi sahihi ya dawa za moyo.
Mhe. Hajati Mwasa alisema kuna kila sababu ya kuendelea kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa aliyoifanya ya kuboresha sekta ya afya katika mkoa wa Kagera kwa kupeleka mashine mpya na za kisasa zinazotusaidia wananchi kupata matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa., Bukoba.
“Mashine zilizopo zimewasaidia pia wataalamu wa JKCI kutoa huduza za uchunguzi kwa urahisi kwani vifaa wamevikuta hapa na vingine wamekuja navyo, hivyo nitoe rai kwa wananchi wa mkoa wa Kagera kuendelea kufika hapa hospitali kufanyiwa vipimo vya magonjwa ya moyo na kujua hali zenu”, alisema Mhe.Hajati Mwasa.
Aidha, ameupongeza na kuushukuru uongozi pamoja na madakatari bingwa kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kufika katika mkoa wa Kagera ili kutoa huduma za vipimo mbalimbali vya magonjwa ya moyo huku akiwasihi kuendelea kuutembelea mkoa huo mara kwa mara na kuwasaidia wananchi kupata huduma hizo.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge, daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka JKCI Yona Gandye aliushukuru uongozi wa mkoa wa Kagera kwa kuwapokea na kuwakubalia kutoa huduma ya uchunguzi na matibabu ya moyo kwa wananchi.
Dkt. Gandye alisema JKCI imekuwa na utaratibu wa kuwafauata wananchi mahali walipo na kutoa huduma ya tiba mkoba ijulikanayo kwa jina la Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services ambayo imewezesha kuwafikia wananchi wengi na kupata huduma za matibabu kwa wakati tofauti na ambavyo wangezifuata huduma hizo JKCI.
“Tangu tumeanza kutoa huduma hizi tumeshafika katika mikoa 12 ya Tanzania bara na Visiwani na huu ni mkoa wa 13, tumeshafanya upimaji wa aina hii katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Arusha, Geita, Mtwara, Lindi, Dodoma, Iringa, Manyara,Kilimanjaro na Visiwa vya Unguja na Pemba”.
“Wananchi 10,807 walifanyiwa vipimo kati ya hao 4375 walikutwa na magonjwa mbalimbali ya moyo ikiwemo shinikizo la juu la damu (BP), kutanuka kwa misuli ya moyo, kuziba kwa mishipa ya damu ya moyo, matundu kwenye moyo, valvu za moyo na mishipa ya damu ya moyo kutokukaa katika mpangilio wake. Wagonjwa 1323 tuliwapa rufaa ya kuja kutibiwa katika Taasisi yetu na tayari wengine wameshakuja na kupatiwa matibabu ya kibingwa”, alisema Dkt. Gandye.
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Bukoba Dkt. Museleta Nyakiroto alimshukuru mkuu wa mkoa wa Kagera Hajati Fatma Mwasa kwa kufungua kambi hiyo ya utoaji wa huduma za kibingwa huku akisisitiza kuwa lengo la kambi hiyo ni kusogeza huduma karibu na wananchi ili kuwapunguzia adha ya kufuata huduma hizo katika mikoa ya mbali ukiwemo mkoa wa Dar es Salaam na Mwanza.
Dkt. Museleta Nyakiroto alisema katika kambi hiyo wananchi wanapata huduma zote za vipimo ya mayo huku akisisitiza kuwa mnamo mwezi Aprili 08, 2024 wanategemea kuwa na kambi nyingine ya madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Kanda ya Bugando watakaokuja kutoa huduma kwa watoto wenye matatizo ya vichwa vikubwa na mgongo wazi.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Yona Gandye akizungumza na wananchi waliofika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Bukoba (BRRH) kwa ajili ya kupata huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa BRRH wakati wa ufunguzi wa kambi maalumu ya siku tano ya uchunguzi na matibabu ya moyo ambapo hadi sasa watu 288 wameshapata huduma za matibabu
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Nuru Letara akiwaelekeza madaktari wa watoto wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Bukoba (BRRH) jinsi ya kufanya kipimo cha kuangalia moyo unavyofanya kazi na kutambua tundu lililopo kwenye moyo wakati wa kambi maalumu ya siku tano ya uchunguzi na matibabu ya moyo inayofanyika BRRH.
Baadhi ya wakazi wa mkoa wa Kagera wakimsikiliza mkuu wa mkoa huo Mhe. Hajati Fatma Mwasa wakati wa ufunguzi wa kambi maalumu ya siku tano ya uchunguzi na matibabu ya moyo inayofanywa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Bukoba (BRRH).