Bukoba. Mfumo wa Unununuzi wa Mazao kwa njia ya Mtandao unaoedeshwa na Soko la Bidhaa Tanzania (TMX), umeongeza ushuru wa mapato mkoani Kagera kwa zaidi ya asilimia 200.
Kwa misimu miwili Serikali kupitia Soko la Bidhaa Tanzania (TMX), imeanza utekelezaji wa ununuzi wa Bidhaa kwa zao la Kahawa mkoani humo ili kuongeza tija katika kilimo hiko.
Akizungumza mjini hapa, Katibu Tawala Msaidizi anayesimamia Uchumi wa Mkoa wa Kagera, Isaya Sendega alisema kabla ya mfumo huo Manisapaa ilikuwa ikikusanya ushuru wa Sh1. 2 bilioni kwa mwaka..
“Mwaka.2023 tukaingia katika mfumo mapato yakapanda mpaka kufikia Sh2. 6 bilioni na mwaka 2024 tayari tumeshakusanya Sh4. 6 bilioni.
Kwa mujibu wa Sendega, mfumo huo umepunguza malalamiko kwa wakulima na kurahisisha ukusanyaji wa ushuru.
Alisema kazi ya kukusanya ushuru sasa imekuwa rahisi hakuna kukikimbizana kwa kuwa kila kitu kipo katika mfumo.
Awali Afisa Mipango wa TMX, Eva Msangi alisema mpango huo wa manunuzi kupitia mfumo wa mtandao katika zao la Kahawa umetekelezwa kuanzia msimu wa mwaka 2022/2023 na 2023/2004.
Msangi alisema tathimini inaonyesha kuwa wakulima na wanunuzi wanaufurahia mfumo huo kwani umerahisisha kupata fedha zao kwa wakati.
Alisema mwaka 2018/2019 huo ulikuwa na changamoto kubwa ya soko la kahawa jambo lilochangia bei kuporomoka kwa kasi huku wakulima wengine waliamua kung’oa miche ya kahawa na kupanda ndizi pekee.