Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
JESHI la Polisi mkoani Pwani, limepunguza uhalifu kwa makosa 259 sawa na asilimia 23.4 ukilinganishwa na mwaka 2020 ambapo kulikuwa na makosa 1,104 dhidi ya makosa 845 ya mwaka 2023.
Aidha mkoa huo ,umefanikiwa kukamata makosa 1,437 kwa mwaka 2023 ikiwa ni makosa yaliyohusiana na madawa ya kulevya kama heroine, bangi ,mirungi ,pombe haramu ya moshi (gongo),nyara za Serikali na ukamataji silaha.
Hayo aliyaeleza ,Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Pius Lutumo ofisini kwake ,wakati alipokuwa akiwaeleza waandishi wa habari kuhusu mafanikio yaliyopatikana ndani ya miaka mitatu tangu Rais Samia Suluhu Hassan na Amiri Jeshi Jeshi aingie madarakani.
Alieleza, mkoa huo ilikuwa ukisumbuliwa na changamoto ya usumbufu wa uhalifu wa wizi wa mifugo lakini kwasasa kuna ahueni.
Lutumo alisema ,mwaka 2020 kulikuwa na makosa 294 dhidi ya makosa 174 kwa makosa ya mwaka 2023 ikiwa ni pungufu ya makosa 120 sawa na asilimia 41.
Kadhalika alieleza ,katika ukamataji wa makosa umeongezeka kwa ongezeko la ukamataji wa makosa 735 sawa na asilimia 104.
Alifafanua, mwaka 2020 yalikamatwa makosa 702 ukilinganisha na makosa 1,437 mwaka 2023.
“Ukifanya tathmini kwenye makosa yanayotokana na misako na operesheni utaona kuna ongezeko la ukamataji kwa makosa 735 sawa na asilimia 104”
“Ifahamike kwamba huu ni ukamataji wa makosa yaliyohusiana na madawa ya kulevya ya Viwandani kama heroine, lakini pia madawa ya kulevya ya mashambani mfano bangi,mirungi, pombe haramu ya moshi,nyara za Serikali na silaha haramu” alisema Lutumo.
Upande wa vitendea kazi ,anasema mkoa umepata magari saba ya doria kati ya hayo mawili ni kwa ajili ya huduma za jamii na safari za masafa marefu.
Lutumo alieleza pia, makazi ya askari polisi yameboreshwa ambapo Mkuu wa Majeshi ametoa milioni 300 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha polisi huko wilayani Kisarawe.
Kamanda huyo alisema, asilimia zaidi ya 80 maofisa ,wakaguzi na askari a vyeo mbalimbali wamepata mafunzo hayo kuongeza ujuzi na kupandishwa vyeo.
Kuhusu matumizi ya TEHAMA, Lutumo anasema hivi sasa wameimarisha mawasiliano ya Tehama na mifumo ya E Ofisi na mifumo mingine kusoma, bila kuwa n majalada au makarini.