Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe, Geophrey Pinda akimpokea Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) Mhe, Japhet Hasunga mara baada ya kamati hiyo kuwasili Kata ya Ibadakuli halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kukagua mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) katika eneo hilo tarehe 20 Machi 2024.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) Mhe, Japhet Hasunga na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe, Geophrey Pinda wakiangalia zoezi la uwekaji alama wakati Kamati ya PAC ilipokwenda kukagua utekelezaji mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi katika halmashauri ya manispaa ya Shinyanga tarehe 20 Machi 2024.
Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhandisi Anthony Sanga akitoa maelezo mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ilipotembelea mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi katika kata ya Ibadakuli halmashauri ya manispaa ya Shinyanga tarehe 20 Machi 2024.
Baadhi ya wananchi wa kata ya Ibadakuli katika halmashauri ya manispaa ya Shinyanga wakihudumiwa wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ilipotembelea mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi katika kata ya Ibadakuli halmashauri ya manispaa ya Shinyanga tarehe 20 Machi 2024. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)
……………
Na Munir Shemweta, SHINYANGA
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe, Geophrey Pinda ameziagiza halmashauri zote nchini zilizokopeshwa fedha kwa ajili ya programu ya kupanga, kupima na kumilikisha ardhi (KKK) kutafuta vyanzo vingine vya fedha kwa ajili ya kuzirejesha ili halmashauri nyingine zinufaike na mkopo huo.
Mhe Pinda alitoa kauli hiyo leo tarehe 20 Machi 2024 mkoani Shinyanga wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ilipotembelea na kukagua utekelezaji mradi wa Uimarishaji Usalama wa Milki za Ardhi nchini (LTIP) katika katika Kata ya Ibadakuli.
Kauli ya Mhe, Pinda inafuatia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kutaka kujua hatua zinazochukuliwa na wizara baada ya kuelezwa kuwa, halmashauri ya manispaa ya Shinyanga ni mojawapo ya halmashauri zilizopewa fedha hizo ambapo ilipata shilingi bilioni 1.055 na kushindwa kuzirejesha kwa mujibu wa makubaliano.
“Halmashauri zote nchini zitafute vyanzo vingine kwa sababu hili jambo limeulizwa mara kadhaa na kama wizara tumeeleza mkakati tunaoenda nao” alisema Mhe, Pinda.
Kwa mujibu wa mhe Pinda, wizara yake kwa sasa haiangalii tena malengo ya mradi katika kupata fedha na badala yake inaenda mbali zaidi ili halmashauri zitumie vyanzo vingine kulipa deni na wakati huo halmashauri hizo zikitumia vyanzo vingine kupata fedha.
Ameitaja halmashauri ya wilaya ya Chalinze iliyopo mkoa wa Pwani kuwa, itakuwa halmashauri ya mfamo kwa kuwa tayari imeonesha nia ya kulipa deni inalodaiwa la shilingi Bilioni 2.5 kupitia vuanzo vingine.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) Mhe Japhet Hasunga amesema kamati yake itaenda kulishuggulilia suala hilo la kusuasua kwa halmashauri kurejesha mikopo ya programu ya KKK na kuona namna ya kulishauri Bunge juu ya suala hilo.
Ameeleza kuwa, msingi mkubwa wa serikali kutenga fedha za mkopo kwa ajili ya mradi wa KKK ni kutaka programu hiyo kuwa endelevu na mwisho wananchi waweze kupatiwa hati milki za ardhi.
“Tunataman kila kipande cha ardhi yetu ipangwe, ipimwe na kumilikishwa na ikianyika hivyo ndiyo tutaona thamani ya ardhi yetu” alisema Mhe, Hasunga.
Akielezea kuhusu mradi wa uboreshaji usalama wa milki za ardhi (LTIP) uliotembelewa na Kamati hiyo ya PAC, mhe, Pinda amesema mradi huo katika halmashauri ya manispaa ya Shinyanga ulianza oktoba 2024 kwa lengo la kurasimisha vipande vya ardhi 20,000 ifikapo juni 30, 2024.
Amesema, hadi sasa vipande vya ardhi 21,850 vimetambuliwa , vipande 7,175 vimepangwa na viwanja 1,315 vimepimwana kwa ujumla kazi hiyo imetekelezwa kwa asilimia 51 na kazi ikiendelea.
Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) ulibuniwa na wizara ya ardhi ili kutatua changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikiikabili sekta ya ardhi kwa muda mrefu. Changamoto hizo ni pamoja na mabadiliko ya teknolojia katika utekelezaji wa kazi za sekta na utoaji huduma za ardhi, kukosekana kwa miundombinu wezeshi ya TEHAMA katika ofisi za ardhi pamoja na kasi ndogo ya upangaji, upimaji na umilikishaji ardhi.