Dkt. Elikana Kalumanga, Meneja Ushirikishwaji wa Sekta Binafsi wa Mradi wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) wa Tuhifadhi Maliasili akiwasilisha mada ya uhifadhi wa wanyamapori
Dastan Kamanzi, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Media Foundation (TMF), akiongea na waandishi wa habari wakati wa mafunzo
Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET), Dk. Ellen Otaru akiongoza mjadala wakati wa mafunzo
………………
NA SIDI MGUMIA, BAGAMOYO
Ushirikishwaji wa wadau mbalimbali katika masuala ya uhifadhi unapaswa kupewa kipaumbele ili kusaidia juhudi za uhifadhi wa wanyamapori na mazingira kwa ujumla.
Ushirikishwaji huo unapaswa kuwagusa wadau wote wa mazingira ikiwemo jamii ili kuleta maendeleo endelevu ya maliasili zilizopo.
Hayo yamesemwa na Meneja Ushirikishwaji wa Sekta Binafsi wa Mradi wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) wa Tuhifadhi Maliasili Dkt. Elikana Kalumanga alipokuwa akizungumza wakati wa mafunzo kwa waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali nchini yaliyofanyika mjini Bagamoyo mkaoni Pwani.
Dkt. Kalumanga amesema ushirikishwaji wa wadau mbalimbali katika uhifadhi na ulinzi wa wanyamapori ni muhimu na utasaidia kulinda wanyamapori, na kwakuliona hilo wao tayari wameshaanza kushirikisha jamii na matokeo chanya yameanza kuonekana.
“Ushirikishwaji wa jamii zinazozunguka hifadhi unapaswa kupewa kipaumbele, na sisi kwa kupitia mradi wa USAID Tuhufadhi Maliasili tumekuwa tukielimisha jamii, na katika miradi tuliyoifanya tayari wameanza kuona faida inayopatikana kutokana na kuishi karibu na hifadhi na wananufaika kupitia fursa mbalimbali zilizopo,” alisema Dkt. Kalumanga
Dkt. Kalumanga alisema kupitia mradi huo wameona fursa kama vile biashara, uhifadhi, kilimo, ufugaji wa nyuki na hata jamii husika sasa inaaminika katika taasisi za kifedha, jambo ambalo awali halikuwepo.
Aidha, Dkt. Kalumanga amesema maeneo ya hifadhi yana faida katika kulinda vyanzo vya maji ambayo yanatumika kwa jamii yote, hivyo hakuna njia mbadala katika hilo tofauti na kuhakikisha kasi ya kuhifadhi mazingira inaongezeka.
“Uhifadhi una faida nyingi ikiwemo kuongeza viumbepori, maji, hali ya hewa nzuri na mengine, hivyo hakuna namna ambayo unaweza kufanya uhifadhi uwe endelevu bila kushirikisha wadau wote zikiwemo sekta binafsi,” amesema.
Kwa upande mwingine Dkt. Kalumanga ameshauri jamii na wadau wengine kuendelea kushirikiana kuhifadhi, kutunza mazingira na wanyamapori ili vizazi vijavyo viweze kurithi na kufaidika na rasilimali hizo ambazo zinaanza kutoweka.
Akiongelea juu ya uandishi wenye tija katika masuala ya uhifadhi, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Media Foundation (TMF), Dastan Kamanzi amewashauri waandishi wa habari kuandika habari za uhifadhi na mazingira kwa kuzingatia katiba, sera, sheria, kanuni, miongozo, mipango na mikakati iliyopo.
“Waandishi wa habari wanapaswa kuandika habari zenye uchunguzi wa kina zenye tija na maslahi kwa umma zenye kutumia akili sana kwa kuzingatia taratibu muhimu za uandishi ili kuweza kuelimisha jamii ipasavyo lakini pia kuhimiza uwazi na uwajibikaji kwa ajili ya ustawi wa maendeleo ya jamii,” alisema Kamanzi
Naye Mwenyekiti wa JET, Dk. Ellen Otaru amewataka waandishi wa habari kuendelea kushirikiana na jamii lakini pia serikali pamoja na wadau wengine wa mazingira, wawe mstari wa mbele kuibua na kuelimisha jamii juu ya athari zitokanazo na shughuli za uhifadhi ili kuleta mabadiliko chanya katika jamii.
“Waandishi wa habari bado wana jukumu kubwa katika suala hili ikiwa ni pamoja na kuendelea kuitumia vyombo vyao vya habari pia mitandao ya kijamii kuzielimisha jamii juu ya tatizo lililopo na namna yakulikabili,” alisema Dk Otaru
JET wamekuwa wakiandaa mafunzo mbalimbali ya masuala ya uhifadhi wa wanyamapori kwa waandishi wa habari za mazingira kwa ufadhili wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) kupitia mradi wake wa Tuhifadhi Maliasili. Ikiwa ni sehemu ya mradi huo wamefanya mafunzo ya siku mbili (Machi 14 na 15 2024) kwa waandishi wa habari zaidi ya 20 mjini Bagamoyo, mkoani Pwani kwa ajili ya kuwaongezea uwezo na kuwahamasisha kuandika masuala yanayohusiana na masuala ya uhifadhi wa wanyamapori.