Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na kikosi kazi cha madini cha taifa linawashikilia watuhumiwa kumi wote wakazi wa Ilomba Jijini Mbeya kwa tuhuma za kusafirisha na kutorosha vipande vya madini aina ya dhahabu.
Watuhumiwa walikamatwa Machi 16, 2024 huko maeneo ya VETA Ikulu, Jijini Mbeya wakiwa na vipande 314 vya madini aina ya dhahabu vyenye uzito wa gramu 9,622.76 sawa na thamani ya shilingi 1,515,621,987.03 bila kuwa na kibali cha kusafirisha madini hayo.
Aidha, watuhumiwa walikutwa na vifaa vingine ambavyo ni vipimo vya dhahabu, majiko, mitungi ya gesi na kasiki ya kuhifadhi fedha.
Watuhumiwa wamekuwa wakitorosha madini hayo kupitia njia zisizo rasmi kwa lengo la kukwepa kulipia kodi, ushuru na gharama nyingine zinazohitaji kwa wafanyabiashara ya madini.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa wito kwa wafanyabiashara ya madini kufuata taratibu ikiwa ni Pamoja na kukata vibali vya kufanya biashara hiyo na kulipa gharama zinazohitajika ili kuepuka usumbufu na hasara pindi wanapobainika kufanya biashara bila kufuata utaratibu.
Imetolewa na:Benjamin Kuzaga – SACPKamanda wa Polisi, Mkoa wa Mbeya.