Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko (kulia)
akimpongeza Askofu Mpya wa Jimbo jipya Katoliki la Mafinga, Mhashamu
Vincent Cosmas Mwagala mara baada ya kuwekwa Wakfu na Kusimikwa kwa
Askofu huyo Mpya wilayani Mufindi mkoani Iringa.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko
(katikati) na viongozi wengine wakiwa katika Sherehe ya kuwekwa Wakfu
na Kusimikwa kwa Askofu Mpya wa Jimbo jipya Katoliki la Mafinga,
Mhashamu Vincent Cosmas Mwagala zilizofanyika Halmashauri ya Mafinga
wilayani Mufindi mkoani Iringa. Wa Pili kushoto ni Naibu Waziri wa
Uchukuzi, Mhe. David Kihenzile, Wa Tatu kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa
Iringa, Peter Serukamba na wa pili kulia ni Spika Mstaafu, Mama Anna
Makinda.
……………………..
*Asema Rais Samia anaendelea kutoa ushirikiano kwa madhehebu ya Dini
*Asisitiza utunzaji wa mazingira
*Amsifu Dkt. Samia kwa kuendesha nchi kwa utulivu na kasi ya maendeleo
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko
amemwakilisha Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Sherehe ya kuwekwa
Wakfu na Kusimikwa kwa Askofu Mpya wa Jimbo jipya Katoliki la Mafinga,
Mhashamu Vincent Cosmas Mwagala na kueleza kuwa Dkt. Samia anaendelea
kutoa kila aina ya ushirikiano kwa Kanisa Katoliki na madhahebu
mengine ili kuwaletea maendeleo Watanzania.
Amesema, nia ya Rais, Dkt. Samia ni kuona wananchi wanapata huduma
bora katika nyanja mbalimbali ikiwemo Zahanati, Barabara, Maji, Shule
na Umeme wa uhakika hivyo ili kutekeleza suala hilo kwa ufanisi
Serikali inashirikiana na Taasisi binafsi ikiwemo madhehebu mbalimbali
ya dini katika kuwapelekea maendeleo wananchi. n.k
Akizungumza na Wananchi waliohudhuria sherehe hiyo katika Halmashauri
ya Mafinga, Wilayani Mufindi mkoani Iringa, Dkt. Biteko amesisitiza
kuhusu utunzaji wa mazingira na kutoa angalizo kuwa yeyote anayeharibu
mazingira lazima aonekane kama adui na achukuliwe hatua kwani athari
za kutokutunza mazingira ni kubwa, akitolea mfano kuwepo kwa mgawo wa
umeme kutokana na kutokuwa na maji ya kutosha kuzalisha umeme.
“Leo tumejenga mradi mkubwa wa umeme wa Julius Nyerere, mradi ule ni
mkubwa sana, lile si bwawa tu bali ni ziwa kwani urefu wake ni
kilometa 100 na upana wake ni kilometa 25, uwepo wake unahitaji maji
na ikizingatiwa kuwa gharama nyingi zimetumika kujenga mradi huo zaidi
ya shilingi Trilioni Sita, ni lazima tulinde mazingira ili kupata
faida mbalimbali ikiwemo maji ya kutosha kuzalisha umeme.” Amesema
Dkt. Biteko
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amesema kuwa tarehe 19 Machi, 2024,
Rais, Dkt. Samia ametimiza miaka mitatu akiwa madarakani ambapo
amedhihirisha kwa vitendo kuwa ni kiongozi bora ambaye ameendelea
kuiweka nchi katika hali ya utulivu.
Ameongeza kuwa, Rais, Dkt. Samia ameendelea kutekeleza miradi
mbalimbali aliyoikuta mara baada ya kuapishwa ikiwemo barabara, reli,
umeme na ameendelea kubuni miradi mipya na kuiendeleza kwa kasi kubwa.
Dkt. Biteko ametoa wito kwa viongozi wa Dini na Watanzani kumuombe
Rais Samia ili aendelee kuongoza nchi kwa ufanisi akiwa na afya njema
na pia kuiombea nchi ili iendelee kuwa ni mahali salama pa kuishi.
Kuhusu uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Dkt. Biteko ametoa wito kwa
Watanzania kuchagua viongozi wanaokerwa na shida za wananchi na
wanaozitatua na kwamba wasichague viongozi kwa kigezo cha ukabila,
dini au mahali walipotoka bali msingi uwe ni maendeleo na utanzania.
Kwa upande wake, Askofu Mpya wa Jimbo la Mafinga, Mhashamu Vincent
Mwagala amesema Kanisa Katoliki litaendelea kutoa ushirikiano kwa
Serikali katika masuala ya ya ustawi wa jamii ili amani iendelee
kutamalaki na kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa miradi ya
maendeleo.
Pia amemshukuru Dkt. Biteko kwa kuhudhuria sherehe hiyo na kuwasilisha
ujumbe wenye matashi mema kutoka kwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Viongozi mbalimbali waliohudhuria sherehe hiyo ni pamoja na Mkuu wa
Mkoa wa Iringa, Peter Serukamba, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David
Kihenzile na Spika Mstaafu, Mama Anna Makinda.