Na Sophia Kingimali
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo wamekagua na kuridhishwa na Maendeleo ya ujenzi wa jengo la Utawala katika Taasisi ya Utafiti wa Viwanda na Maendeleo (TIRDO) huku wakitoa rai kwa taasisi hiyo kuanza kujiendesha kibiashara ili waweze kujitegemea
Akizungumza leo Machi 18,2024 jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari mara baada ya kukagua ujenzi huo Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Deodatus Mwanyika amesema serikali imeongezea uwezo wa kimiundombinu TIRDO ambao walikuwa na majengo chakavu ambayo hayakuwa yanaenda na taasisi hiyo.
Amesema kuwa Serikali kupitia Wizara hiyo iridhihinisha jengo la utawala litengenezwe kwani jengo hilo halijakamilika kwa muda mrefu wa miaka 40 sasa tangu kuanza kujengwa.
“Jengo hili limeanza muda mrefu sana tangu 1984 na hapo katikati lilisimama sasa mnatakiwa likaimilike ili lianze kutumika kibiashara. Wizara muone haja ya kuwatumia watifiti wenu waliopo TIRDO kibiashara kama chanzo cha mapato,” Mwanyika.
Amesema wizara inapaswa kusimamia taasisi zake na kuhakikisha bajeti inayopangwa inatolewa kwa wakati ili kukamilisha mipango iliyowekwa. Hata wakichelewa kukamilisha hawana haja kuwalaumu TIRDO bali wizara husika ambayo pesa zinapitia kwao.
Aidha Mwanyika ameshauri kuwa wizara kuweka kitengo ndani ya Shirikisho kwaajili ya ushauri wa kibiashara ii waweze kujitegemea wasiwe tegemezi.
Pia Kamati ya kudumu ya bunge imeitaka wizara ya viwanda na biashara kuhakikisha kuwa jengo hilo linakamilika kwa wakati uliopangwa ili watafiti waweze kufanya kazi zao katika mazingira mazuri na ya biashara
Kwa upande wake Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Ashatu Kijaji amesema ujenzi wa jengo hilo la utawala linatarajia kutumia kiasi cha shilingi bilioni 3.4 ambapo mpaka sasa wameshapokea shilingi bilioni 1.54
“Ili jengo likamilike bado tuna nusu fedha tunaendelea kuomba serikalini fedha kwa bajeti ijayo kukamilisha ujenzi huu hadi sasa umefikia asilimia 72 za mradi umebaki asilimia 28 na ujenzi huu unatarajia kukamilika June 30 mwaka huu,”amesema Dk. Kijaji.