Serikali ya Tanzania na Italia zimeahidi kuimarisha ushirikiano katika sekta za kimkakati ambazo ni kilimo, nishati, elimu pamoja na uchumi wa buluu kwa maslahi ya pande zote mbili.
Ahadi hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbaouk (Mb.) alipokutana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Italia, Balozi Riccardo Guariglia wakati wa Iftari iliyoandaliwa na Ubalozi wa Italia nchini Tanzania jana jioni.
Balozi Mbarouk ameipongeza Serikali ya Italia kwa kuipa Serikali ya Tanzania kipaumbele cha kuwa moja kati ya nchi nne za Bara la Afrika zitakazonufaika na mpango mpya wa kimkakati wa Mattei (Mattei Plan). “Tanzania tunaamini kuwa kupitia mpango wa Mattei ushirikiano wa kiuchumi kati yetu na Italia utazidi kuimarika,” alisema Balozi Mbarouk.
Balozi Mbarouk aliongeza kuwa mpango wa mattei utainua sekta za kimkakati ambazo ni kilimo, nishati, elimu na uchumi wa buluu kwa upande wa Zanzibar, Sekta hizi zimepewa kipaumbele kufuatia umuhimu wake katika kukuza uchumi.
Pamoja na masuala mengine Tanzania imeihakikishia Italia ushirikiano katika kuunda kamati ya kuratibu mpango wa mattei ambayo itahakikisha sekta za kimkakati zilizoainishwa katika mpango huo zinananufaika kama ilivyopangwa kwa maslahi ya pande zote mbili.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Italia, Balozi Riccardo Guariglia alisema kuwa Italia ni rafiki wa Tanzania wa muda mrefu na mataifa hayo yamekuwa yakishirikiana katika sekta mbalimbali. Hivyo mpango wa Mattei ni moja ya njia za kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi baina ya Italia na Tanzania na Afrika kwa ujumla.
“Tupo hapa kuonesha na kuhakikisha kuwa Tanzania inanufaika na mpango wa mattei, lakini pia kuiona Afrika ikifanikisha kuweka vipaumbele vya malengo na kutekeleza majukumu yake kupitia mpango wa mattei kwa ufanisi,” alisema Balozi Guariglia
Balozi Guariglia aliongeza kuwa lengo la mpango wa mattei ni kuendelea kuimarisha uchumi wa Bara la Afrika kwa kuzishirikisha sekta za umma na binafsi za Italia katika kufadhili mpango huo kwa maslahi ya pande zote mbili.
Mwezi Januari 2024, baada ya kumalizika kwa mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika na Italia, serikali ya nchi hiyo iliahidi kutuma ujumbe wa wataalam kutoka Chemba ya Biashara ya Italia kuja Tanzania kwa ajili ya kukutana na timu ya wataalam ya upande wa Tanzania kwa lengo la kukamilisha hatua za awali za utiaji saini wa ushirikiano za kutekeleza mpango wa mattei.
Aidha, katika kutekeleza hilo, mwezi Machi 15, 2024 Ujumbe wa Italia ukiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Ushirikiano wa Maendeleo katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ya Italia, Mhe. Stefano Gatti ulikutana na timu ya wataalamu wa Tanzania na kuainisha sekta za kipaumbele zitakazo nufaika na mpango mpya wa kimkakati wa Mattei (Mattei Plan).