Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (LAAC), wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti Mheshimiwa Stansalus Mabula, wakikagua ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Misenyi mkoani Kagera.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (LAAC), akieleza jambo mbele ya watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Misenyi wakati Kamati hiyo ilipotembelea na kukagua ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri hiyo.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (LAAC), pamoja na wajumbe wa Kamati hiyo wakiangalia mashine ya mionzi (x-rays) wakati Kamati hiyo ilipotembelea na kukagua ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Misenyi.
Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (LAAC), wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti Mheshimiwa Stansalus Mabula, wakiwaangalia wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Kitobo Wilaya ya Misenyi waliokuwa wanatoa maelezo ya viumbe hai na wanyama katika maabara ya bailojia wakati Kamati hiyo ilipotembelea na kukagua ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Misenyi mkoani Kagera.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (LAAC), akizungumza wakati Kamati hiyo ilipotembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa Shule ya Sekondari Kitobo iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Misenyi.
…………
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali imeutaka uongozi wa Mkoa wa Kagera kuwasilisha taarifa za hospitali za Halmashauri zote katika Mkoa huo ambazo zinaidai Bohari ya Dawa (MSD), tangu mwaka 2021.
Agizo hilo limetolewa na Makamu mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mheshimiwa Stansalaus Mabula wakati Kamati ilipotembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Misenyi.
Wakati Kamati inakagua mradi huo ilibaini kwamba pamoja na kwamba mradi huo umeshakamilika kwa asiliamia kubwa lakini bado MSD haijawasilisha vifaa vya zaidi ya shilingi milioni 400.
“Tunaomba kesho kabla Kamati haijaondoka katika Mkoa wa Kagera, RAS (Katibu Tawala wa Mkoa), tupate taarifa ya madeni katika Halmashauri zote ambazo inaidai MSD, haya majengo yakikaa miaka miwili bila kutumia yataharibika.
“Karibu kila Kamati ya Bunge inailalamikia MSD, wana madeni makubwa na yanazalisha hoja za kiuchunguzi kila siku,” alisema.
Kwa upande wake, akizungumza kwa niaba ya Kamati, mjumbe wa Kamati hiyo, Mheshimiwa Daimu Mpakate aliitaka Halmshauri ya Wilaya ya Misenyi kufanya utafiti wa kimazingira katika maeneo ya Halmshauri hiyo yalikojengwa majengo ya Serikali kwa kuwa maeneo hayo yametawaliwa na unyevu mwingi.
“Mkurugenzi wekeni hii katika bajeti zenu za kawaida, bila kufanya hivi baadae katika miaka ijayo mtajikuta majengo yote haya yanatitia ardhini, TAMISEMI Wilaya hii inahitaji mtaalamu wa mazingira ili kafanya tathimini ya kimazingira ” alisema.
Kamati pia ilitembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Kitobo iliyopo katika Halmashauri hiyo na kuelekeza kurekebisha hatua ya ukamilishaji (finishing) vizuri zaidi.
Aidha, kwa ujumla alipongeza kazi kubwa na nzuri iliyofanywa ya ujenzi wa majengo katika miradi yote miwili katika Halmashauri hiyo.
Kamati ya LAAC kesho inatarajia kukagua mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba na baadae itasafiri kuelekea Mkoa wa Geita.