Kukosekana kwa elimu sahihi ya kulipa kodi ya ongezeko la thamani VAT kwa baadhi ya wafanyabiashara kwenye Halmashauri ya Wiaya ya Same imetajwa kuwa sababu mojawapo inayochangia baadhi yao kukwepa kulipa kodi pindi maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania wanapopita kwenye maduka yao kukusanya mapato.
Wakizungumza kwenye kikao cha Mkuu wa Wilaya ya Same Kasilda Mgeni baadhi ya wafanyabiashara hao wameiomba Serikali kupitia kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA kutoa elimu ya namna ya kulipa kodi hiyo kwa wafanyabiasara kuepukana na usumbufu usio wa lazima unaojitokeza wakati wa kulipa kodi.
Akijibu kero na malalamiko ya wafanyabiashara hao Mkuu huyo wa Wilaya amewataka TRA kukaa meza moja na wafanyabiashara hao kufanyia kazi malalamiko yaliyowasilishwa kwao ili kuwezesha kuwa na uelewa wa pamoja utakao saidia kumaliza changamoto ya baadhi ya wafanyabiashara kukwepa kulipa kodi ya ongezeko la thamani.
Kufanyika kwa kikao hicho ni muendelezo wa vikao vya Mkuu wa Wilaya ya Same kusikiliza na kutatua kero na malalamiko ya makundi mbali mbali ndani ya Wilaya hiyo ili kuwezesha wananchi kuweza kutekeleza shughuri za maendeleo kwenye maeneo yao kwa amani na usalama.