Wakazi wa Kijiji cha Tungamalenga kilichopo katika Tarafa ya Idodi wilayani Iringa wameishukuru serikali kwa kuendelea kuwawezesha kiuchumi ambapo wameeleza kunufaika na shilingi Milioni 57 ambazo zimetolewa kupitia Mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW) kama fedha mbegu wanazoweza kukopeshana na kuendesha shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Baadhi ya Wakazi wa kijiji hicho ambao wanaoishi pembezoni mwa hifadhi ya Taifa Ruaha wamesema fedha hizo zimewasaidia kuboresha maisha na kuweza kuondokana na hali duni ya maisha kwani hujiunga katika vikundi na kupatiwa fedha mbegu ambazo huzitumia kuanzisha miradi mbalimbali ambayo hukubaliana inayowasaidia kujiingiza kipato.
Katibu wa Kikundi cha Kordun kutoka jamii ya Kimaasai Janeth Matambile ambacho ni kimojawapo kinachonufaika na mradi huo amesema fedha mbegu wanazopatiwa zimewasaida kukopeshana na kuendeleza miradi mbalimbali waliyoianzisha ikiwemo unenepeshaji wa ng’ombe.
“Tulipatiwa fedha mbegu ambazo zimetusaidia kujenga mabanda ya ng’ombe ya kisasa kwa lengo la kuwanenepesha, mradi wa REGROW pia umetusaidia kuondokana na dhana potofu kuwa wanawake ni wa kukaa nyumbani tu na kwa sasa wanawake wanajishughulisha katika usindikaji wa maziwa na kutengeneza Sanaa”-Alieleza Janeth.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Tungamlenga Bw. Linus Mheluka amebainisha kuwa mradi huo ulianza kwa mafunzo yaliyotolewa kwa vikundi ambayo yamechagiza kuhakikisha fedha zilizotolewa zinatumika ipasavyo.
“Mradi wa REGROW katika Kijiji changu cha Tungamalenga ulianza katika mwaka wa fedha 2021/22 na ulianza kutoa mafunzo kwa vikundi alafu wakatoa mikopo. Sasahivi nina vikundi saba ambavyo vimeshapatiwa fedha mbegu takribani shilingi Milioni 57 kwa lengo la kukopeshana na kumekuwa na mabadiliko ya kiuchumi kwao”-Alieleza Bw. Mheluka.
Mheluka ameongeza kuwa mradi wa REGROW umetoa mafunzo kwa vijana wa Kijiji hicho kupitia ngazi mbalimbali za vyuo ambapo shilingi Milioni 113 zimetolewa kufadhili masomo kwa wanafunzi 29 katika Kijiji hicho huku pia Askari 10 wa Wanyamapori ngazi ya Kijiji wakisomeshwa pia fedha za miradi kiasi cha shilingi Milioni 178 zimetolewa kwa vikundi sita, mpaka sasa mradi huo umetoa jumla ya zaidi shilingi Milioni 371 katika Kijiji hicho.
Kwa upande wake Afisa Uhifadhi anayesimamia mradi wa REGROW katika Hifadhi ya taifa Ruaha Bw. Priscus Mrosso amesema vijiji zaidi ya 84 vinavyoizunguka hifadhi hiyo vinanufaika na mradi huo ambapo mpaka sasa shilingi Milioni 820 zimetolewa kwa vijiji vitano katika awamu ya kwanza hatua inayosaidia kuisogeza jamii karibu kwa kunufaika na hifadhi hiyo na kuweza kuwa chachu ya kuimarisha ulinzi kwa kupunguza matukio ya ujangili.
Mabadiliko kwa wakazi wa kijiji cha Tungamalenga yameonekana kwani kupitia mradi wa REGROW baadhi yao wameweza kutumia vema fursa ya uwezeshwaji huo kusomesha watoto, kuendesha shughuli za kilimo, ufugaji pamoja na kufanya biashara.