VIJANA Nchini wametakiwa kuwafichua wafanyabiashara wasio waadilifu ambao wanadiliki kuihujumu Serikali kwa kuwauzia wananchi Sukari kwa bei ya juu ambayo si bei elekezi.
Hayo yamebainishwa na Makamu Mwenyekiti wa UVCCM Taifa Rehema Sombi wakati akifungua mkutano mkuu wa UVCCM vyuo na vyuo vikuu Taifa unaofanyika mkoani Iringa katika chuo cha Ihemi kinachomilikiwa na UVCCM.
Akizungumza na vijana kutoka vyuo mbalimbali Nchini, Sombi alieleza kuwa, vijana wanapaswa kuwa askari namba moja wa kuibua vitendo vinavyofanyika kwenye jamii ambavyo vinamuumiza mwananchi moja kwa moja.
Alisema wapo baadhi ya wafanyabiashara anaouza bidhaa ikiwemo sukari kwa kujipangia bei zao wenyewe huku wakiwaumiza wananchi na kupelekea wananchi kuichukia Serikali yao pamoja na chama kinachoingoza Serikali,chama cha Mapinduzi CCM.
“Ndugu vijana,kumekuwepo na ukiukwaji wa taratubu zilizowekwa na Serikali juu ya bei elekezi ya sukari Nchini, wapo wafanyabiashara ambao siyo waaminifu kwa maksudi wamekuwa wakiihujumu Serikali kupandisha bei ya Sukari, wanaofanya watambue kuwa wana ihujumu Serikali” Alisema Sombi.
Katika hatua nyingine, Sombi alieleza kuwa katika uhai wake hayati mwalimu Julius Kambarage Nyerere alishawahi kusema”Bila CCM madhubuti Nchi itayumba, lakini umoja wa vijana unaendelea kuyaamini maneno hayo kwa vitendo na kusema kuwa bila ya UVCCM madhubuti CCM itayumba, hivyo ni muhimu vijana kujibidiisha katika majukumu yao kwa manufaa ya chama na Taifa kwa ujumla.