Na.Jacob Kasiri – Dar es Salaam.
Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limenogesha safari ya Afrika Kusini kwa kukabidhi mipira ya mazoezi kwa Timu ya Taifa ya Mpira wa Pete (Tanzania Princess) inayotarajia kuondoka nchini kesho terehe 15.03.2024 kuelekea nchini Afrika Kusini kushiriki Michuano ya Kimataifa ya Mpira wa Pete kwa wachezaji walio chini ya umri wa miaka 20, katika hafla fupi iliyofanyika leo Machi 14, 2024 katika Uwanja wa Taifa wa Benjamin Mkapa (Lupaso) uliopo jijini Dar es Salaam.
Akitoa mipira katika hafla hiyo Afisa Uhifadhi Mkuu Mohamed Kiganja kutoka TANAPA alisema, “Mipira hii ninayoikabidhi kwenu leo ilete hamasa na kujituma mazoezini ili mfanikiwe kuleta ushindi kwa Watanzania. Vilevile niwasihi mtakapokuwa huko peperusheni Bendera ya Taifa huku mkinadi vivutio vyetu kama alivyofanya Rais wetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, mkifanya hivyo mchango wenu pia utaonekana katika sekta ya utalii kama ambavyo mchango wenu umeshajipambanua katika sekta ya michezo.”
Naye, Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Pete (Netball) Devota Marwa alisema, “Niwashukuru TANAPA kwa kutuunga mkono kwa kutupatia mipira ya mazoezi, licha ya mipira hii pia tutaondoka na baadhi ya vipeperushi vinavyoonyesha vivutio vyetu ili tukaitangaze vyema Tanzania kwa lengo la kuvutia watalii wengi zaidi kutembelea vivutio hivyo.”
Aidha, Nahodha wa Timu ya Taifa ya Mpira wa Pete (Tanzania Princess) Catherine Bunzari wakati akipokea mipira hiyo aliwahakikishia Watanzania kurudi na ushindi na kuongeza kuwa, “Chapa ya TANAPA katika mipira hii tunayokabidhiwa ni ishara ya deni kubwa kwetu, hivyo kila tutakavyocheza na kuliona neno TANAPA litatukumbusha kutangaza vivutio vya utalii vilivyomo ndani ya Hifadhi za Taifa.”
Ili kuendelea kutangaza vivutio vyake na fursa za uwekezaji zinazopatikana ndani ya Hifadhi za Taifa 21, TANAPA wanaendelea kuyafikia maeneo ya kimkakati hususani michezo ya kimataifa ili kufikia adhma ya serikali ya kupata watalii milioni 5 na mapato ya Dola za Kimarekani bilioni 6 ifikapo 2025/2026.