Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia Ombeni Manase Kilawa [43] mkazi wa Lusese Wilaya ya Mbarali anayetuhumiwa kumuua mke wake aitwaye Happynes Gervas Mwinuka [40] mkazi wa Kijiji cha Lusese kwa kumkata na kitu chenye ncha kali.
Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia Machi 13, 2024 Kitongoji cha Masista, Kijiji cha Lusese, Wilaya ya Mbarali baada ya kutokea ugomvi baina ya wana ndoa hao wakiwa nyumbani kwao na kupelekea mtuhumiwa Ombeni Kilawa kuchukua kisu na kumkata mke wake shingoni.
Uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha tukio hilo ni wivu wa kimapenzi baada ya mtuhumiwa kumhisi na kumtuhumu mke wake kuwa na mahusiano ya kimapenzi na wanaume wengine.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya, linatoa wito kwa jamii kuwa pindi wanapopatwa na tatizo au changamoto katika ndoa zao isiwe suluhisho lake kujichukulia sheria mkononi bali ni kutafuta ushauri kwa wazazi, walezi, wasimamizi wa ndoa, viongozi wa dini, katika madawati ya jinsia na watoto waliopo kila Wilaya ya Kipolisi, katika ofisi za halmashauri au kutafuta haki kwenye Mahakama ili kuepuka madhara.
Imetolewa na:
Benjamin Kuzaga – SACP
Kamanda wa Polisi,
Mkoa wa Mbeya.