Asifa uhusiano na masoko mfuko wa huduma za Afya ZHSF Asha Kassim Biwi akijenga uelewa Kwa watendaji wa Tume ya Ukimwi Zanzibar huko Ofisi za tume hiyo kwamchina wilaya ya magharibi B.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya usimamizi na Ubora wa huduma kutoka ZHSF Habiba Sultan Mbwana akijenga uelewa Kwa watendaji wa Tume ya Ukimwi Zanzibar huko Ofisi za tume hiyo kwamchina wilaya ya magharibi B.
PICHA NA FAUZIA MUSSA-MAELEZO ZANZIBAR
Na Takdir Ali na Rahma Khamis. Maelezo.
Wanachama wa Mfuko wa huduma za Afya Zanzibar (ZHSF) watakaochangishwa pesa katika Vituo vya Afya na Hospitali wametakiwa kutoa taarifa ili wahusika wachukuliwe hatua za kisheria.
Wito huo umetolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya usimamizi na Ubora wa huduma kutoka ZHSF Habiba Sultan Mbwana wakati alipokuwa akitoa maelezo katika kikao cha utoaji wa elimu kwa Viongozi na Wafanyakazi wa Tume ya Ukimwi Zanzibar (ZAC) huko Mombasa Wilaya ya Magharibi B.
Amesema kuna baadhi ya Watoa huduma wanawatoza fedha Wateja wao kwa madai ya kuchangia baadhi ya gharama za Dawa,Vipimo na matibabu jambo ambalo ni kinyume na Taratibu za Mfuko huo.
Amefahamisha kwa Mteja yoyote wa ZHSF anapokwenda katika Vituo vya Afya na Hospitali zilizosajiwa na Mfuko huo hatakiwa kutoa pesa yoyote kwani tayari wameshasaini Mkataba maalum wa kutoa huduma zote za Afya ya Msingi.
Aidha amesema Mtu yoyote anapohitaji matibabu ya dharura anatakiwa kupatiwa katika hositali au kituo cha afya kilichokaribu nae na yoyote atakayeshindwa kuhudumia Wateja wanaohitaji matibabu ya dharura atachukuliwa hatua kwa mujibu wa Sheria ikiwemo kusitisha Mkataba wake.
Mbali na hayo Dkt. Habiba amesema Serikali haitomvumbia macho Mtoa huduma yoyote atakaebainika kumtolesha pesa kwa ajili ya gharama za Dawa, Matibabu au Vipimo kwani watoa huduma hao wameasaini Mkataba na ZHSF wa kutoa huduma bora kwa Wananchi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa kinga na Uratibu kutoka Tume ya Ukimwi Zanzibar (ZAC) Bwana Sihaba Saadat Haji ameishauri ZHSF kuweka saini za alama za Vidole kwa wanaopatiwa huduma ili kuzuia kufanyiwa ubadhirifu Mfuko huo.
Hata hivyo ameipongeza ZHSF kwa kutoa elimu hiyo kwani imeweza kuwapa mwanga wa kufahamu masuala mbalimbali yaliokuwa yaliokuwa yanawasumbua wakati wanapofika Hospitali au Vituo vya Afya kupata matibabu.
Nao Wafanyakazi wa Tume ya Ukimwi Zanzibar (ZAC) wameiomba ZHSF kulipatia ufumbuzi tatizo la kutakiwa kuchangia pesa katika vituo vya afya na hospitali na kutopatiwa matibabu ya dharura hasa wakati wa usiku jambo ambalo linawapa usumbufu mkubwa.