Mkemia Mkuu wa Serikali  Zanzibar Dkt. Farid Mzee Mpatani akitoa taarifa ya kitaalam kufuatia Vifo vya watu 9  vinavyosadikiwa kusababishwa na kula nyama ya kasa machi 6 huko kisiwa panza kisiwani Pemba, hafla iliyofanyika Wizara ya Afya Mnazimmoja Zanzibar

Naibu waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Hassan Khamis Hafidh akitoa tamko kwa vyombo vya habari kufuatia vifo vya watu 9  vinavyosadikiwa kusababishwa na kula   nyama machi 6 huko kisiwa panza kisiwani Pemba, hafla iliyofanyika Wizara ya Afya Mnazimmoja Zanzibar

Naibu Mkurugenzi kinga na elimu ya afya Fatma Kabole akitoa ufafanuzi wa vifo vya watu 9  vinavyosadikiwa kusababishwa na kula   nyama ya kasa machi 6 huko kisiwa panza kisiwani Pemba, hafla iliyofanyika Wizara ya Afya Mnazimmoja  Zanzibar

PICHA NA FAUZIA MUSSA – MAELEZO ZANZIBAR

Na Rahma Khamis Maelezo. 

Serikali kupitia Wizara ya Afya Zanzibar  imewataka wananchi kuacha kula nyama ya kasa ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza ikiwemo kifo.

Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari huko Ofisini kwake Mnazimmoja  Naibu waziri wa wizara hiyo Mhe Hassan Khamis Hafidh amesema hatua hiyo imekuja  kufuatia vifo vya watu tisa  na wengine 18 kulazwa katika Hospitali ya Abdalah Mzee kati ya watu 160 waliokula nyama hiyo inayosadikiwa kuwa na sumu.

“  watu tisa wamefariki kutokana na kula nyama hiyo na zaidi ya watu 15  kulazwa katika Hospitali Abdallah Mzee ” Alifahamisha naibu waziri

Aidha Wizara inatoa pole kwa wale wote waliofikwa na msiba na  waliopata  madhara na kuwataka wananchi kuacha kabisa kula nyama ya kasa  ili kuepuka madhara yatokananyo na nyama hiyo.

“Kutokana na Utafiti uliyofanywa kitaalamu na kubainika kuwa na nyama hiyo kua na  sumu na kupelekea kifo” alifahamisha.

Akitoa taarifa ya kitaalam  Mkemia Mkuu wa Serikali Faridi Mzee Mpatani amesema kitaalamu kuna  aina saba za kasa ambapo katika aina hizo,  aina nne za kasa kuna baadhi ya vyakula wakila wanadamu humsababishia maradhi ama kifo.

Ameeleza kuwa  kwa kushirikiana  na Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali ya Tanzania Bara wamefanya uchunguzi wa kitaalamu na   kubaini uwepo wa sumu katika nyama hiyo na kusema  kuwa sumu hiyo inahimili joto ambapo  hata ikipikwa haiwezi kuondoka.

Aidha ameongeza kuwa sumu hiyo kitaalamu inajuulikana kwa jina la telenikostizim ambayo husababisha madhara katika mfumo wa mwanadamu  ikiwemo kuhisi kichefuchefu, homa na baadae kufariki.

Kwa upande wake Naibu Mkurugeni Kinga na Elimu ya Afya Fatma Kabole amefahamisha kuwa watoto hao waliofariki wapo chini ya umri wa miaka kumi na wanatoka katika familia tofauti ndani ya Kisiwa panza huku Serikali ikiendelea kufuatilia wengine ili kuwabaini waliotumia nyama hiyo na kuwapatia matibabu.

Amefahamisha kuwa jumla ya watu 160 wanasadikiwa kula nyama hiyo katika kisiwa hicho na kuitaka jamii kuwapeleka katika vituo vya afya kwa uchunguzi na kupatiwa matibabu.

 Itakumbukwa kwamba mnamo tarehe 6 Machi kuliripotiwa taarifa za tukio hilo lililotokea  katika Kisiwa Panza Mkoa wa kusini  Pemba.