…….
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameihakikishia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuwa Serikali itahakikisha inasimamia ukarabati na uboreshaji wa Kiwanja cha Ndege cha Tabora ili kukamilika ifikapo mwezi Oktoba, 2024.
Bashungwa ameyasema hayo Machi 13, 2024 mkoani Tabora katika ziara ya Kamati hiyo ya kukagua maendeleo ya mradi huo na kusisitiza Wizara kupitia Wakala ya Barabara (TANROADS), itahakikisha inamsimamia Mkandarasi wa kampuni ya Beijing Construction Engineering Group (BCEG), kufanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha kazi hiyo kwa ubora.
“Mheshimiwa Mwenyekiti na Wajumbe wa Kamati, niwadhihirishie kuwa kutokana na baadhi ya changamoto zilizojitokeza katika mradi, tutamsimamia Mkandarasi ili atukabidhi mradi mwezi Oktoba mwaka huu”, amesema Bashungwa.
Aidha, Bashungwa ameeleza kuwa moja ya sababu ya miradi kuchelewa ni kutokana na Taasisi za Serikali kutoshirikiana kwa karibu katika maandalizi na utekelezaji wa mradi na amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi kushiriana na Makatibu wakuu wengine katika uratibu wa utekelezaji wa miradi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Selemani Kakoso (Mb) amemuagiza Waziri Bashungwa kuhakikisha anamsimamia Mkandarasi anayejenga na kukarabati Kiwanja cha Ndege cha Tabora kufanya kazi kwa ufanisi na ndani ya muda uliopangwa.
Kadhalika, Kakoso amemtaka Bashungwa kufuatilia upatikanaji wa fedha za utekelezaji wa miradi kwa wakati ili kuwawezesha Wakandarasi wanaotekeleza miradi nchini kupokea malipo yao kwa wakati yatakayofanikisha ukamilishaji wa miradi kulingana na mikataba.
Naye, Kaimu Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Eng. Doroth Mtenga ameeleza kuwa ujenzi na ukarabati wa Kiwanja hicho umefikia asilimia 38 na unahusisha ujenzi wa jengo la abiria lenye uwezo wa kuhudumia abiria 120 kwa wakati mmoja, ofisi mbalimbali, sehemu za biashara, ujenzi wa mnara wa kuongoza ndege na ujenzi wa barabara wa kuingia na kutoka kiwanjani.