Baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA Wilaya ya Njombe kubaini uwepo wa risiti feki walizopewa wananchi wa kata ya Iwungilo kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha Afya na michango mingine,Mkuu wa wilaya ya Njombe amelazimika kuwaita viongozi wa Chama hicho na kusikiliza changamoto hiyo.
Katika kikao hicho kilichoongozwa na Mkuu wa wilaya ya Njombe Kissa Kasongwa na kamati yake ya Ulinzi na Usalama pamoja na Viongozi wa CHADEMA Chini ya mwenyekiti wao wa mkoa Rose Mayemba na baadhi ya wananchi wa Iwungilo kimebainisha namna ya kuchukua hatua dhidi ya Malalamiko ya wananchi hao.
Awali viongozi wa Chadema Rose Mayemba na Regnard Danda wamesema katika kata ya Iwungilo mbali na changamoto ya Risiti feki lakini kuna malalamiko mengi ya Wananchi dhidi ya Viongozi wa Vijiji na Kata ambayo hatua za haraka zinapaswa kuchukuliwa.
Baadhi ya wananchi wa Iwungilo wakiwemo waliolipishwa michango na kupewa risiti feki akiwemo Gustaf Mtewele Betina Mgina na Melsiana Mtewele wamesema vitendo wanavyofanyiwa huko kijijini vinawakwaza pakubwa na kuiomba serikali kuchukua hatua dhidi ya viongozi hao.
Akizungumza kwa Niaba ya mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa Njombe bwana Izack Mapunda amekiri kuwa risiti hizo sio za halmashauri ya mji na kwamba wataenda kufanya ukaguzi kuona matumizi ya fedha hizo.
“Tuliwaruhusu kutumia hizi Ila zitakuja kutolewa za halmashauri pindi kitabu kitakapofika,alisema mapunda”
Kwa upande wake mkuu wa Wilaya ya Njombe Kissa Kasongwa amekiri kuziona risiti hizo bandia na kwamba atakwenda kufuatilia kuona uhalisia wake na kuchukua hatua stahiki.