Na: Dk. Reubeni Lumbagala, Kongwa, Dodoma.
Tarehe 8 Machi kila mwaka, Tanzania inaungana na nchi nyingine kote duniani kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani ambapo kwa mwaka 2024, maadhimisho hayo yanaongozwa na kaulimbiu isemayo “Wekeza kwa Wanawake Kuharakisha Maendeleo ya Taifa na Ustawi wa Jamii.” Mwanamke ni mwanajamii muhimu katika juhudi za maendeleo katika jamii yeyote ambapo bila mchango wa mwanamke masuala mengi ya kimaendeleo yanakwama.
Uwepo wa Siku ya Wanawake duniani, ni jitihada ambazo Umoja wa Mataifa (UN) umezifanya katika kuhakikisha changamoto cha wanawake katika nyanja zote za kijamii, kiuchumi na kisiasa zinajadiliwa na kutafutiwa suluhisho la kudumu ili kuhakikisha kunakuwepo na usawa wa kijinsia na hivyo wanawake kunufaika na fursa mbalimbali za maendeleo zilizopo katika jamii na nchi kwa ujumla. Kwahiyo, Siku ya Wanawake Duniani sio siku ya kula, kunywa na kusherehekea peke yake, bali ni pamoja na kufanya tafakuri ya kina kuhusu mafanikio, changamoto za wanawake ili kufikia usawa wa kijinsia ambao ni muhimu katika maendeleo.
Somo ambalo nimedhamiria kulitoa leo kwa wanawake popote walipo hapa nchini ni kuelewa kuwa hakuna namna ambayo jitihada za wanawake zinaweza kufikiwa kama wanawake wenyewe hawatashirikiana kwa pamoja kuhakikisha malengo yao waliyojiwekea yanafikiwa kwa wakati. Mathalani, hakuna namna ambayo wasichana na wanawake watafanikiwa kielimu kama wao wenyewe hawaoni umuhimu wa kusoma kwa ajili ya kujiletea ukombozi wao wenyewe, jamii na taifa lao .
Kama wanawake wanataka usawa wa kijinsia na maendeleo ya kweli wakati huo huo wakipuuza elimu, ni ngumu kwao kufanikiwa. Badala yak e wanaume wataendele kuwa juu ikiwa wanaume wana juhudi kubwa katika kusoma na kutafuta elimu kwa nguvu zao zote.
Kisiasa; mkombozi wa wanawake kuhakikisha wanawake wanashiriki katika ulingo wa siasa na hatimaye kushika nyadhifa mbalimbali za kiuongozi kunategemea sana utashi wa wanawake kushiriki katika siasa bila kusubiri msukumo kutoka kwa wanaume juu ya ushiriki wao wa masuala ya kisiasa.
Wanawake wenyewe waone umuhimu wa kugombea nafasi mbalimbali za kiuongozi ili lengo ya kuwa na wastani wa 50/50 kati ya wanaume na wanawake liweze kufikiwa bila kutegemea uwepo wa viti maalum katika ngazi za udiwani na ubunge. Ikiwa wanawake watakosa uthubutu na kujiamini juu ya uwezo mkubwa walionao kiuongozi, wanaume wataendelea kushika nyadhifa mbalimbali za kiuongozi huku wanawake wakitegemea nafasi za uteuzi kwa kiasi kikubwa.
Katika kuchangamkia fursa mbalimbali za kiuchumi, bado upo uzito wa wanawake kuziona na kuzichangamkia fursa mbalimbali za kiuchumi zilizopo katika maeneo mbalimbali. Wanawake wasisubiri kuletewa taarifa kuhusu uwepo wa mikopo ya wanawake inayotolewa na Halmashauri zote nchini, bali wao wenyewe wawe sehemu ya kufuatilia mikopo hiyo na waitumie katika kujiletea ukombozi wa kiuchumi kwa maendeleo endelevu ya familia zao na Taifa.
Halikadhalika, zipo fursa za mikopo zinazotolewa na taasisi mbalimbali za fedha kwa ajili ya wanawake, hivyo basi, wanawake wasisubiri kutangaziwa juu ya kuunda vikundi vya wanawake ili kukopeshwa, bali wanawake wenyewe waunde vikundi na kuwasilisha taarifa za vikundi vyao kwenye taasisi za kifedha ili waweze kunufaika na mikopo hiyo, hatimaye waweze kukuza biashara na shughuli zao nyingine za ujasiriamali.
Wanawake wanafanya kazi kubwa na wanashirki kikamilifu katika shughuli mbalimbali ikiwemo kilimo, uchimbaji Madini, biashara n,k hapa nchini na kuchangia asilimia kubwa ya shughuli za maendeleo kutokana na ushirki wao chanya wenye kuleta tija kwa shughuli za kiuchumi
Mafanikio haya ya ushiriki wa wanawake katika shughuli za maendeleo, yanapaswa kuonekana katika nyanja nyingine pia ili kukata kiu ya wanawake ya kufikia usawa wa kijinsia wa 50/50.
Upo umuhimu mkubwa wa wanawake kutiana moyo wao kwa wao kuwa wanaweza kufanya mambo makubwa ya kimaendeleo bila kusubiri mchango wa wanaume ili kufikiwa kwa malengo ya wanawake. Utamaduni mbaya wa kukatishana tamaa miongoni mwa baadhi ya wanawake ni kikwazo kikubwa cha kufikiwa malengo ya wanawake.
Wanawake wawe mstari wa mbele kuhamasishana wenyewe kwa wenyewe kuwania nafasi mbalimbali za kiungozi. Mwanamke aliyefanikiwa kiuchumi aone fahari kuwasaidia wanawake wenzake ambao bado wako nyuma ili nao waweze kufikia viwango alivyofikia yeye na hata zaidi kwani maendeleo ya watu wengi yana tija kubwa katika maendeleo ya Taifa.
Mafanikio ya wasichana na wanawake yanategemea sana juhudi za wanawake wenyewe kujikomboa. Hakuna namna ambayo nchi yetu itafanikiwa katika hili kama wanawake wenyewe watabaki nyuma huku wakitegemea huruma na msaada wa wanaume kuwezeshwa. Yote katika yote, wasichana na wanawake wasisahau wala wasipuuze umuhimu wa kusoma kwa bidiii kwani elimu ndiyo chemchem ya mafanikio. Wanawake takakarini, mchukue hatua.
Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi mahiri wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan umewekeza na kutoa fursa za kutosha kwa wanawake ili kuweza kupiga hatua za kimaendeleo. Kazi iliyobaki ni wasichana na wanawake kujitambua na kuzitumia vyema fursa hizo ili kufikia maendeleo endelevu.
Dk. Reubeni Lumbagala ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Mlali iliyoko wilaya ya Kogwa mkoani Dodoma. Maoni: 0620 800 462.