Na Mwandishi wetu, Simanjiro
MKUU wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Dkt Suleiman Hassan Serera, ameendelea na ziara yake ya kutembelea kitongoji kwa kitongoji kwa lengo la kusikiliza kero na changamoto za jamii.
Dkt Serera, akizungumza na waandishi wa habari, amesema lengo la ziara yake ni kuhakikisha wakazi wa vitongoji vyote 278 wanafikiwa na kusikilizwa ii kutatua matatizo yao.
“Katika ziara yangu naambatana na wataalamu mbalimbali wakiwemo wa idara ya afya, elimu, ardhi, maji, barabara na wengineo hivyo watu wakiwa na kero au changamoto zao wanapatiwa majawabu,” amesema.
Dkt Serera amesema ataendelea na ziara hiyo kwa kutembelea kitongoji kwa kitongoji kwa lengo la kuwasikiliza wakazi husika na kuzungumza nao ili kuendelea kujenga Simanjiro.
Amewapongeza wakazi wengi wa vitongoji husika kushiriki mikutano hiyo na kuzungumza kero na changamoto zinazohusu jamii kwa ujumla na siyo matatizo binafsi.
Diwani wa kata ya Endiamtu, Lucas Chimba Zacharia, ametoa shukrani kwa Dkt Serera, kwa kufanya ziara ya kitongoji kwa kitongoji na kusikiliza kero za wakazi wa eneo hilo.
“Hii ni mara ya kwanza kwa mkuu wa wilaya kufika ngazi ya kitongoji na kitongoji na kusikiliza kero za jamii na kuhakikisha zinazoweza kutatuliwa zinatatuliwa kwa wakati,” amesema.
Diwani wa kata ya Emboreet, Yohana Shinini amemshukuru mkuu huyo wa Wilaya kwa kuwatembelea na kuwasikiliza kwani changamoto na kero za vitongoji zimepata ufumbuzi.
“Hongera sana mkuu wetu kwa ziara yako kwenye kata ya Emboreet, kitongoji kwa kitonji, kwani matatizo ya jamii yamepata majawabu na utatuzi wa wa kero umefanyika,” amesema Shinini.
Mkazi wa kitongoji cha Kairo, Shiwarael Nyari (Gaakona) mwenye umri wa miaka 70, amemshukuru Dkt Serera kwa namna alivyoweza kuwasaidia kwa kuingilia kati tozo ya jengo kupitia luku.
“Huwa tunakatwa fedha ya tozo ya jengo pindi tukilipia ankara ya nishati ya umeme kwa njia ya luku, tunamshukuru Mhe DC amewasiliana na watu wa mamlaka ya mapato (TRA) ili tuondolewe hiyo tozo,”amesema Nyari.