Waziri wa biashara na maendeleo ya Viwanda Omar Said Shaaban akitoa taarifa ya bei elekezi ya kuuzuia sukari katika kipindi cha mwezi mtukufu wa ramadhani ,huko ofisini kwake Kinazini Mjini Unguja.
PICHA NA FAUZIA MUSSA-MAELEZO ZANZIBAR
Na Sabiha Khamis Maelezo
Serikali kupitia Wizara ya Biashara na viwanda imetoa bei elekezi ya kuuzia sukari katika kipindi cha mfungo wa Ramadhani ili kuwapunguzia wanachi gharama za matumizi katika mwezi huo.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari huko ofisini kwake Kinazini Wilaya ya Mjini, waziri wa wizara hiyo Mhe. Omar Said Shaaban amesema hatua hiyo imekuja kufuatia agizo la Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi alilolitoa hivi karibuni katika ziara yake ya kutembelea wafanyabiashara na kusikiliza changamoto zao.
Katika Ziara hiyo Rais wa Zanzibar aliitaka wizara ya Biashara kutoa bei elekezi ya kuuzia sukari baada ya serikali kuondoa gharama za VAT katika bidhaa hiyo ili kupunguza makali ya maisha hasa katika kipindi cha mwezi mtukufu wa ramadhani.
Amesema kufuatia agizo hilo wizara ya Biashara imeelekeza wafanyabiashara wote kushusha bei ya sukari katika kipindi cha ramadhani na kuuza kwa shilingi 2,650 kwa kilo moja kwa upande wa Unguja na shilingi 2,700 kwa kilo kwa upande wa Pemba.
Akizungumzia bei elekezi kwa wauzaji wa jumla amesema bidhaa hiyo itauzwa kwa shilingi 123,000 upande wa Unguja na Shilingi 126,000 kwa upande wa Pemba ambapo waingizaji wa bidhaa hizo watauza kwa shilingi 121,000 kwa upande wa Unguja na shilingi 124,000 kwa upande wa Pemba kwa ujazo wa kilo 50.
Amefahamisha kuwa bei hizo zimezingatia utoaji wa kodi na faida kwa kila mmoja hivyo amewataka wafanyabiashara hao kutekeleza agizo hilo na kueleza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mfanyabiashara yoyote atakaekwenda kinyume na agizo hilo ikiwemo kufutiwa leseni ya biashara.
Aidha amewataka watendaji wa Tume ya Ushindani Halali ya Biashara kutekeleza wajibu wao na kuhakikisha sukari inauzwa kwa bei elekezi katika kipindi chote cha mwezi mtukufu wa Ramadhan mpaka itakapotangazwa vyenginevyo.
Wakati huohuo Waziri Shaaban , amewaomba wafanyabiashara kutopandisha bei kwa bidhaa ambazo hazijatolewa bei elekezi na kuweka unafuu kwa wananchi ili kumudu gharama za mwezi huo.
“Hiki si kipindi cha kuchuma faida nyingi za kifedha ni kipindi cha kuchuma thawabu hivyo tuwe na mazingatio na tukumbuke kwamba tunatoa unafuu kwa wananchi wenzetu” alisema Mhe. Omar.
Mhe. Shaaban amewaomba Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Masheha kuisaidia Serikali katika kuhakikisha dhamira ya Mhe. Rais ya kuwasaidia wananchi katika kipindi cha Ramadhani na kuhakikisha wanapata mahitaji yao kwa bei nafuu inafikiwa .
Kabla ya Serikali kutangaza bei elekezi sukari iliuzwa zaidi ya shilingi elfu tatu kwa kilo moja ndani ya Zanzibar.