Na Sophia Kingimali
Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Albert Chalamila amemtaka mkandarasi anaejenga barabara ya Kimara Mavurunza mpaka sengerea yenye thamani ya bilion 24.03 kuhakikisha anamaliza ujenzi huo kama mkataba wake unamvyomtaka lakini pia kuhakikisha anatoa ajira kwa vijana wa jimbo la ubungo na Segerea.
Akizungumza leo March 9,2024 wakati wa Hafla ya kumkabidhi mkandarasi barabara hiyo amesema barabara hiyo ilikuwa ni kilia cha muda mrefu kwa wakazi wa bonyokwa.
“Hii barabara imekuwa ni kilio cha muda mrefu kwa wakazi wa eneo hili tulikuja hapa kipindi mvua zilivyonyeesha wananchi wakatununia lakini ilikuwa ni wajibu wao kufanya hivyo sasa wakati wakufurahi umefika,”Amesema.
Amesema mkandarasi anapaswa kufanyakazi usiku na mchana ili kuhakikisha barabara hiyo inakamilika ndani ya miezi 16 na kuahikisha pindi mvua zitakaponyeesha ikute barabara imeanza na inakaribia kukamilika ili wananchi wasipate usumbufu.
Aidha Chalamila amesema amepata taarifa kuwa kunabaadhi ya wakazi wa eneo hilo wameishtaki TANROAD hivyo amesema wataendelea kusikiliza maamuzi ya mahakama na pindi hukumu ikitoka kama TANROAD imeshinda basi atachukua hatua za haraka kuhakikisha anaboma nyumba zote kwenye eneo hilo.
“Nimepata taarifa kuwa kuna baadhi ya wakazi wa hapa wameenda kuishtaki TANROAD jambo zuri sana ila niwahakikishie endapo hukumu itatoka TANROAD imeshinda sitachukua hata dakika 10 nitakuwa nimeshafika hapa na kijiko sitaangalia nini kimetoka au nani yupo ndani nitavunja zote”,Amesema.
Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Segerea Bona Kamoli amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuidhinisha pesa kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa barabara hiyo huku akitoa wito kwa serikali kuhakikisha wanakarabati mto Msimbazi kwani umekuwa ukiwafuata wananchi na si wananchi kufuata mto kama ilivyokuwa awali.
Amesema barabara ikikamilika itaongeza uchumu kwa wakazi wa maeneo hayo kwani watakuwa na uwezo wa kufanyakazi muda wote lakini hata watu wataongezeka kwani watakuwa na uhakika wa usafiri.
Naye Mbunge wa jimbo la Ubungo Prof Kitila Mkumbo amesema ujenzi wa barabara hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya CCM kwani hiyo ilikuwa moja ya ahadi ya chama kwa wananchi wake.
Akizungumzia ujenzi wa barabara hiyo Mkurugenzi wa barabara TANROAD Eng.Jephason Nnko amesema ujenzi wa barabara hiyo utahusisha na ujenzi wa daraja la Kinyerezi lakini pia kuwekwa kwa taa barabara yote ili kusaidia hata wafanyabiashara kuweza kufanyabiashara zao wakati wote.
Kwa upande wake meneja mradi kutoka Kampuni ya ujenzi Nyanza Eng.Gilbert Bahesha amesema watahakikisha history inaendelea kuandikwa katika barabara hiyo kwani wanatarajia kumaliza mradi huo kwa wakati uliopangwa ili kuendelea kukata kiu ya wananchi hao.