Na Ashrack Miraji Same Kilimanjaro
WANAWAKE mkoani Kilimanjaro wametakiwa kuchangamkia fursa kipindi cha uchaguzi serikali za mitaa na vijiji kwa kuchukua fomu na kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ili washirikiane kuleta maendeleo.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu leo Februari 8,2024 katika maadhimisho ya siku ya wanawake duniani ambayo kimkoa yamefanyika katika uwanja wa mpira wilayani Mwanga mkoani hapo.
“Nataka niwaombe wanawake mkagombee nafasi za uongozi kwa ngazi hizo najua mheshimiwa Rais ndiye Mwenyekiti wa chama cha Mapinduzi,nategemea wanawake wengi watajitokeza kuchukua fomu na kwa umahiri wenu nina imani mtashinda vizuri”
Amesema kauli mbiu ya mwaka huu ambayo ni “wekeza kwa wanawake ;kuharakisha maendeleo ya taifa na ustawi wa jamii” inachangia kuleta hamasa katika kuleta usawa wa kijinsia na uwezeshaji wananawake wote nchini.
“Kauli mbiu hii inachangia kuleta hamasa katika kujua umuhimu wa ujumuishi wa wanawake katika masuala mbalimbali ya uamuzi ili kuendelea kutimiza ndoto zao katika nyanja za uongozi na kuinua uchumi na kuondokana na unyanyasaji ma ukatili wa aina zote” amesema mkuu huyo wa mkoa.
Aidha Babu amewataka wanawake wanapoadhimisha siku hiyo kila mmoja atafakari ulinzi na usalama wa mtoto suala ambalo amesema limeachwa nyuma na kupelekea watoto kuwa wahanga wakubwa wa vitendo vya ukatili.
Ameiongeza kuwa “Nitoe rai kwa wanawake wote pamoja na jamii kwa ujumla kusimama katika nafasi zao za kuhakikisha watoto wanalindwa na kupata malezi bora na kujengwa katika maadili bora yatakayokuwa mwongozo mzuri kwa taifa letu baadae”
Wakati huohuo Katibu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT),Irimina Mushongi amesisitiza kuwa wanawake wote wawe walezi bora wa watoto wao pamoja na kufanya jitihada za kupunguza ukatili kwa watoto bila kusahau kuchangamkia fursa za uongozi zitakapotoka.
“Mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi wa serikali za mitaa niwasihii kinamama wenzangu kwa sababu mama samia ni rais sisi tunahitaji wanawake wote kugombea nafasi zote tukagombee uenyeviti wa vijiji na serikali za mitaa hatimaye mwakani kieleweke” amesema katibu Mushongi.
Naye katibu Tawala Wilaya ya Same, Upendo Wella kwa niaba ya Katibu Tawala Mkoa wa Kilimanjaro,Tixon Nzunda amesema katika kuadhimisha Siku hiyo hapo awali wamefanya matendo ya huruma kwa kusaidia wasiojiweza na kutoa msaada kwa wahitaji.
“Tumefanya maetendo ya huruma kwa kutoa msaada kwa shule 17 za sekondari kwa kuwapa taulo za kike,sabuni,nguo za watoto,maziwa ya kopo na sukari kwa wanawake walioko gerezani pamoja na kutembelea wodi ya wazazi ya hospitali ya Huruma” amesema Wella.
Hata hivyo inaelezwa kuwa Ushiriki wa Wanawake katika siasa na uongozi bado ni mdogo ukilinganishwa na wanaume nchini, kwani hadi sasa ni asilimia 37 pekee ya wanawake ndio wanaoshika nyadhfa za juu katika ngazi za maamuzi ikiwemo Bunge.