Mabaharia wanawake wa Meli ya New Butiama Hapa kazi Tu katika picha ya pamoja muda mfupi baada ya kuifikisha Meli hiyo salama katika Bandari ya Nansio, kisiwa cha Ukerewe mapema leo tarehe 08.03.2024.
Mabaharia wanawake wa upande wa Injini wakiongozwa na Mhandisi Mkuu Meli ya New Butiama Hapa kazi Tu Bi. Ester Sikazwe (wa pili toka kushoto) muda mfupi baada ya kuifikisha Meli hiyo salama katika Bandari ya Nansio, kisiwa cha Ukerewe mapema leo tarehe 08.03.2024.
Mabaharia wanawake wa upande wa ‘Deck’ (upande wa abiria) wa Meli ya New Butiama Hapa kazi Tu wakiongozwa na nahodha wa meli hiyo Bi. Ester Mniko (katikati) muda mfupi baada ya kuifikisha Meli hiyo salama katika Bandari ya Nansio, kisiwa cha Ukerewe mapema leo tarehe 08.03.2024.
Kaimu Mkurugenzi wa Kampuni yua Huduma za Meli (MSCL) Bi. Neema Mwale (Katikati) akiwa na Nahodha wa meli ya New Butiama Hapa Kazi Tu Bi. Prisca Mniko (Kulia) na Mhandisi Mkuu wa Meli ya New Butiama Hapa kazi Tu Bi. Ester Sikazwe (Kushoto) muda mfupi kabla ya kuanza safari kwa meli ya New Butiama Hapa Kazi Tu.
………..
Wanawake mabaharia wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) wameadhimisha Siku ya Wanawake Duniani kwa aina ya tofauti huku wakiitumia siku hiyo kuonesha uwezo wao wa kuiongoza meli ya New Butiama Hapa Kazi Tu inayofanya safari zake kati ya Bandari ya Mwanza Kaskazini na Bandari ya Nansio, katika kisiwa cha Ukerewe.
Wanawake hao 16 kuanzia ngazi ya nahodha, mhandisi wa meli, pamoja na mabaharia wengine wenye majukumu mbalimbali katika kuiongoza meli wameudhihirishia umma wa watanzania na dunia kwa jumla kuwa wanaweza kuleta maendeleo ya taifa na kuistawisha jamii na kuimarisha pato la taifa.
Mapema akizungumza kabla ya meli hiyo kuondoka katika Bandari ya Mwanza Kaskazini Kaimu Mkurugenzi wa MSCL Bi. Neema Mwale alieleza kuwa Kampuni hiyo imeweka mikakati ya kuwaongezea ujuzi mabaharia hao wanawake na kutoa fursa za ajira kwa wanawake katika sekta ya Ubaharia.
“Tasnia hii kama tunavyofahamu kwa muda mrefu imekuwa ikitawaliwa na wanaume lakini Serikali imeweka msukumo mkubwa sana kwa kuwekeza kwa wanawake na tunaishukuru sana Serikali kwa kuona umuhimu wa kuongeza nguvu katika kuhamasisha wanawake kupata elimu, hivi sasa tunaona kuna mainjinia na manahodha wanawake wapo kwenye meli na siku hii ya leo meli yetu itaendeshwa na wanawake,” Alisema.
Kwa upande wake Nahodha aliyeongoza meli hiyo Bi. Prisca Mniko alieleza kuwa miongoni mwa changamoto za kazi za ubaharia ni pamoja na kuwa mbali na familia kwa muda mrefu hasa unapofanya safari za meli kwa kwenda nje ya nchi, hata hivyo ameshauri kuwa wanawake hawapaswi kuogopa bali waendelee kutimiza majukumu yao katika familia na katika meoneo yao ya kazi.
“Kufanya kazi zilizokuwa zinafanywa na wanaume haimaanishi kwamba wewe ni Tom Boy (Jike dume) ili uwe mama shujaa ufanye kazi zile zilizokuwa zinafanywa na wanaume vile vile ufanye kazi kama mwanamke na utimize majukumu yako kama mwanamke, kama kuzaa uzae kama ni kumhudumia mume wako umuhudumie na uendelee kufanya kazi anazofanya mwanaume,” alisisitiza.
Aidha wakati akihamasisha wanawake kujitokeza kusomea fani ya ubaharia Mhandisi wa meli ya New Butiama Hapa kazi tu Bi. Esther Sikazwe aliwaomba wanawake kuondoa dhana ya kuwa mwanamke kufanya kazi za ubaharia ni kutokuwa na maadili katika jamii na badala yake aliwasihi wanawake kutumia fursa hiyo kujipatia ajira zinatotokana na sekta ya ubaharia inayobeba dhana ya uchumi wa bluu nchini.
“Kwa wazazi na watoto wa kike kote nchini mimi nawaambia njooni kwenye uchumi wa bluu, sekta ya bahari. Wote tunafahamu kuwa uchumi kwa kiwango kikubwa unakuzwa kwa sekta ya bahari katika usafirishaji wa mizigo, hata upatikanaji wa ajira ni nyingi sana, kuna meli nyingi zinazomilikiwa na makampuni mengi na MSCL inakwenda kujenga na kukarabati meli zaidi ya nne, ajira zipo na sasa hivi fani ya ubaharia inawahitaji wanawake,” Alifafanua.
Mabaharia leo tarehe 08.03. 2024 wamefanikiwa kutoka Bandari ya Mwanza Kaskazini asubuhi saa 3:20 na kufika Bandari ya Nansio, Ukerewe saa 5:50 asubuhi meli ya New Butiama Hapa Kazi tu katika siku maalum kwa ajili yao endesha meli yenye uwezo wa kubeba abiria 200 na tani 100 za mizigo.