NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Katika Kusherehekea Siku ya Wanawake Duniani, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imemtambua Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Utalii ya Zara International Travel Agency kutoka Mkoa wa kodi Kilimanjaro Zainab Addan Ansell kuwa Mlipakodi namba moja Mwanamke nchini Tanzania mwaka 2023.
Akizungumza leo Machi 8, 2024 Jijini Dar es Salaam katika maadhimisho ya Siku ya Mwanamke Duniani, Naibu Kamishna Mkuu wa TRA, Bw. Hassan Mcha amesema kuwa ni muhimu watanzania kuwa na utamaduni wa kulipa kodi ili kuleta mabadiliko chanya kwa Taifa.
Mcha amesema kuwa TRA inampongeza Zainab Ansell kwa uzalendo na juhudi katika kufanya kazi ya Utalii na mchango wake wa kipekee kwa kulipa kodi kwa Maendeleo ya Taifa.
“Endelea kung’aa na kuhamasisha wanawake wengine kufuata nyayo zako za mafanikio na kuleta tija” amesema Mcha.
Ametoa wito kwa wanawake wa TRA kuendelea kuwa walinzi wa taswira nzuri ya Mamlaka hiyo kwa kuwa vinara wa uadilifu, weledi, uwajibikaji, na uaminifu katika kutekeleza majukumu yao
“Tuweke taswira nzuri kwa wateja wetu tunaowahudumia, tukijenga mahusiano mazuri na kuongeza ari ya ulipaji kodi, tunatambua wanawake ni Jeshi kubwa, mkaleta mabadiliko katika jamii yetu na kuiwezesha TRA kutimiza malengo yake ya ukusanyaji kodi kwa maendeleo ya taifa letu” amesema Mcha.
Akizungumza niaba ya Wafanyakazi Wanawake wa TRA, Kaimu Mkurugenzi Rasilimali Watu na Utawala, Renalda Lyimo, amesema kuwa wanatambua juhudi zinazofanywa na wanawake wa katika kuhakikisha malengo yanafikiwa.
Lymo amesema kuwa wataendelea kufanya kazi kwa ufanisi ya kukusanya Mapato ya Serikali ili kufikia malengo yenye tija kwa Taifa.
Mwakilishi wa Kampuni ya Utalii ya Zara International Travel Agency, Leila Lakhan ameishukuru TRA kwa kutambua mchango wao wa kulipa kodi kwa Maendeleo ya Taifa.
Ameahidi kuendelea kulipa kodi kwa wakati katika kuhakikisha Taifa la Tanzania linapiga hatua katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Maendeleo.
Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani mwaka huu yamebeba kauli mbiu isemayo “Wekeza kwa Wanawake Kuharakisha Maendeleo ya Taifa na Ustawi wa Jamii”