Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula amemshukuru na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hasan kwa kutatua mgogoro wa ardhi uliodumu kwa muda mrefu kati ya wananchi wa mitaa mitano ya Mhonze B, Nyamwilolelwa, Kihiri, Shibula na Bulyan’hulu inayopatikana kata ya Shibula dhidi ya uwanja wa ndege wa kimataifa wa mkoa wa Mwanza.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya shule ya msingi Nyamwilolelwa MNEC Mhe Dkt Angeline Mabula amesema kuwa Rais Mhe Dkt Samia ameridhia ulipwaji wa fidia ya kiasi cha shilingi Bilioni 19.2 kwa kaya 1404 ambazo zipo katika maeneo yenye mgogoro kama fidia ya maendelezo kufuatia tathimini ya haraka iliyofanywa awali wakati wa kukagua maendelezo ya wananchi katika eneo hilo hivyo kinachosubiriwa ni utekelezaji wa maagizo ya wizara kwa ngazi ya mkoa na wilaya kulingana na taratibu watakazoziweka ili kutatua na kumaliza kabisa mgogoro huo
‘… Niwaombe wananchi kujitokeza na kutoa ushirikiano kwa serikali wakati wa zoezi la uthamini na vikao kwaajili ya kumaliza mgogoro huu, Tujipange vizuri kama kuna sehemu tutakuwa hatujaelewa ni vizuri kuuliza ili watufafanulie na kila mmoja aweze kupata haki yake, Tusitumie lugha chafu wakati wa vikao, Tusiishie kulalamika tu …’ Alisema
Aidha Dkt Mabaula ameongeza kuwa wakati anaingia madarakani mwaka 2015 alikuta migogoro mikubwa ya ardhi isiyopungua 12 ikiwemo ule wa Mhonze, Ilalila eneo la magereza, Lukobe eneo la jeshi, Nyagungulu eneo la jeshi , Zenze viwanja vya wananchi, Kigoto kati ya wananchi na polisi, uwanja wa ndege pamoja na wananchi na fidia kwa watu waliotwaliwa maeneo yao kwaajili ya shughuli mbalimbali za umma hivyo kuishukuru Serikali kumaliza sehemu kubwa ya migogoro hiyo ndani ya jimbo lake.
Kwa upande wake diwani wa kata ya Shibula Mhe Swila Dede amemshukuru mbunge wa jimbo hilo na Rais Dkt Samia Suluhu Hasan kwa uamuzi huo huku akiwataka wananchi wake kuendelea kuwa watulivu wakati taratibu za serikali zikiendelea katika kuutatua mgogoro huo uliodumu kwa muda mrefu.
Nae mwenyekiti wa Serikali ya mtaa wa Kihiri ulio jirani kabisa na uwanja huo wa ndege Bwana Ezekiel Masaki Mafuru amesema kuwa anaishukuru Serikali kwani wananchi wa mtaa wake kwa muda mrefu walisitisha shughuli zao za kujiendeleza kimaisha hivyo kupatikana kwa suluhu ya mgogoro huo kunaenda kufungua ukurasa mpya wa maisha yao sanjari na kuahidi ushirikiano pindi litakapoanza zoezi la uthamini na uhakiki kwaajili ya fidia kwa wananchi wake.
Lucy Iyonza na Specioza Justine ni wananachi wa kata ya Shibula kwa nyakati tofauti mbali na kufurahia maamuzi hayo wameomba uharakishwaji wa zoezi la uhakiki, uthamini na ulipwaji wa fidia pamoja na kuwataka wataalam kuhakikisha hawachukui muda mrefu katika kutekeleza maelekezo ya Rais Dkt Samia Suluhu Hasan ili kumaliza mgogoro huo.