Na Mwandishi wetu
Moshi.
KATIKA juhudi za kuinua kiwango cha michezo mashuleni, Chama cha Soka Mkoa wa Kilimanjaro (KRFA) kimeliomba Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuleta wataalamu watakaowanoa na kuwapiga msasa kwa kuwapa elimu walimu wa michezo shuleni.
Mwenyekiti wa Chama Cha Soka Mkoa wa Kilimanjaro (KRFA),Isaac Munisi “Gaga” ameyasema hayo wakati wa hafla ya ugawaji wa mipira 1000 kwa halmashauri sita mkoani hapa itakayosambazwa mashuleni kwa ajili ya programu ya ‘Football For Schools (F4S).
Hafla hiyo iliyofanyika Machi 7,2024 katika ukumbi wa mkutano uliopo katika ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro ambapo kila halmashauri moja kati ya sita zilizopo mkoani hapa ambazo ni Moshi Mjini,Moshi Vijinini,Mwanga,Same,Hai na Rombo zimepewa mipira 166 itakayosambazwa kuinua michezo mashuleni.
Munisi amesema Wataalamu hao watasaidia kuwanoa walimu katika stadi za michezo, mbinu bora za ufundishaji, na jinsi ya kuibua vipaji vya wanafunzi ambapo elimu hiyo itasaidia kuimarisha michezo mashuleni na kuwawezesha walimu kutoa mafunzo bora kwa wanafunzi.
“Najua kule kuna walimu lakini wengi bado uwezo wao wa kufundisha ni mdogo,wanaweza wakawa wamesoma kufundisha watu wazima lakini si watoto wadogo hivyo elimu inahitajika”
Ameongeza kwa kusema “Kwahiyo ,niwaombe shirikisho watuletee wataalamu walau wapate hata kozi za wiki moja mpaka mbili ili watakapoenda kuwafundisha wanafunzi wajue na kuelewa wanachofundishwa”.
Wakati huohuo Mbunge wa Moshi Mjini,Priscus Tarimo ameweka wazi kwamba serikali itawekeza zaidi katika viwanja na kujenga vituo vya michezo ambapo awali walipanga kujenga kituo wilayani Siha lakini mpango huo ulikwamishwa na ufinyu wa bajeti.
“Viwanja vyetu vitazidi kuwekezwa katika wilaya mbalimbali,tuliwahi kuwa na ndoto za kuwa na kituo cha michezo kule Siha na eneo tukapata lakini tatizo la kibajeti likatukwamisha,” amesema Mbunge Tarimo.
Hata hivyo Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amewaagiza walimu wote waliokabidhiwa mipira hiyo wasijaribu kwenda kuiuza bali wahakikishe inakwenda kufanya kazi iliyokusudiwa na kukuza vipaji vya watoto mashuleni vinginevyo wakibainika sheria kali itachukuliwa dhidi yao.
Kwa upande wake Afisa Taaluma wa Manispaa ya Moshi,Naomi Mhando ameishukuru TFF kuupa kipaombele mkoa wa Kilimanjaro kuwa miongoni mwa mikoa kati ya mikoa 14 (12 ya bara na miwili visiwani) kupata mipira 1000 ambayo itasambazwa mashuleni.
“Kwa mipira hii tutaenda kufanya kitu cha tofauti kabisa,watoto wetu wataenda kuitumia na watafanya vizuri kwenye mashindano ya Umiseta na Umitashumita tutaibuka vinara” amesema Mhando.