Benki ya FINCA Mkoa wa Iringa imewapa zawadi wanawake wafanyabiashara ambao wamekuwa wakifanya vizuri kwenye mikopo wanayopewa.
Wanawake waliopatiwa zawadi hizo ni Otilia Mbonde kutoka Iringa Mjini na Delfina Kipangula maarufu kwa jina la Mama Lawelu, mkazi wa Mafinga.
Delfina na Otilia wamepokea zawadi wakati Benki ya FINCA Iringa ilipoamua kuungana na wanawake katika kuadhimisha siku ya Wanawake Duniani.
Meneja wa FINCA Tawi la Iringa, Phillip Kimbe akikabidhi zawadi kwa wanawake hao amesema huo ni mchango wao kuonyesha namna wanavyo thamini jitihada zao.
“Wanawake wengi wamefanya vizuri, hawa ni miongoni mwao, wamefikia uwezo wa kukopa kiasi chochote wanachotaka na wakapewa kwa muda mfupi. Wanakopa na kurejesha kwa wakati,” amesema.
FINCA ni kati ya taasisi za kifedha ambayo imewafikia wanawake wengi nchini Tanzania na kusaidia mabadiliko yao kiuchumi.
Otilia ameishukuru FINCA kwa kuwawezesha wanawake kwenye mikopo jambo ambalo limesaidia kukuza uchumi.
Kwa upande wake mama Lawelu ameiomba FINCA kuwawezesha wanawake wengi zaidi ili wafikie mafanikio.