Katika kuadhimisha siku ya wanawake Dunia inayoadhimishwa kila ifiikapo Machi 3, Chuo Kikuu Mzumbe kimetoa msaada kwa waathirika wa mafuriko katika Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro wenye thamani ya ShT 4,135,000
Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Allen Mushi akizungumza mara baada ya kukabidhi msaada huo amesema Mzumbe kila mwaka imekuwa na utamaduni wa kugusa jamii katika Nyanja tofauti na mwaka huu wameona ni vyema kuwagusa waathilika wa mafuriko Wilaya ya Kilosa.
“Tumeleta sare za shule kwa watoto wa kike na kiume, madaftari, kalamu na penseli, miswaki na dawa za meno. Vifaa vingine ni pamoja na sabuni za kufulia, taulo za kike na chumvi.” Prof. Mushi aliweka bayana.
Chuo Kikuu Mzumbe kupitia Kituo cha Msaada wa Kisheria kutoka Kitivo cha Sheria kimeendelea kutoa huduma za kisheria bure katika masuala ya mirathi, ardhi, ndoa na masuala mtambuka wilayani hapo ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.
Kwa ipande wake Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Mhe. Shaka Hamdu Shaka ameushukuru uongozi Chuo Kikuu Mzumbe kwa msaada huo na kusisitiza kuwa Wilaya hiyo imekumbwa na mafuriko makubwa toka mwezi Desemba 2023.
“Ninakuhakikishieni kwamba msaada huu utawafikia walengwa na tunakupongezeni sana kwa kutoa msaada wa kisheria kwa siku tatu wilayani kwetu, mwitikio ni mkubwa na ninashauri tuweke utaratibu endelevu wa kusogeza huduma hii kwa wananchi walau huduma hii iwe inatolewa kila mwezi” Amesisitiza Shaka.
Amesema Chuo Kikuu Mzumbe kimechagua mahali sahihi kutoa huduma ya kisheria kwa kuwa Kilosa ni wilaya yenye migogoro mingi ya ardhi, ndoa na mirathi; hivyo, msaada huo ni vema ukawa endelevu ili kutatua changamoto zinazowakabili wakazi wa wilaya hiyo.