Na Mwandishi wetu, Serengeti.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania – TAWA Mej. Jen. (Mstaafu) Hamis Semfuko amewataka Maofisa na askari wa Mapori ya akiba Ikorongo na Grumeti kuongeza umahiri katika utendaji kazi ili kuendana na kasi ya uwekezaji mahiri (SWICA) uliofanyika ndani ya hifadhi hizo zilizoko wilaya za Serengeti na Bunda Mikoa ya Mara na Simiyu.
Semfuko ameyasema hayo Machi 06, 2024 wakati wa ziara ya siku moja ya kutembelea na kujionea shughuli zinazofanywa na TAWA katika hifadhi hizo.
Akizungumza na Maafisa na askari wa Mamlaka hiyo katika eneo la Fort Ikoma, Mwenyekiti huyo aliwasisitiza kuongeza
ushirikiano kati ya TAWA na wawekezaji ikiwemo Kampuni ya Grumeti Fund Trust katika kuhakikisha shughuli za uhifadhi zinaimarishwa.
Alisema Bodi kwa kushirikiana na Serikali wameendelea kufanya maboresho makubwa ndani ya Mamlaka hiyo kwa kuboresha mazingira ya utendaji kazi wa watumishi hasa kuongeza vitendea kazi.
“ Kipindi cha nyuma TAWA ilikuwa katika mazingira magumu, Askari wetu walifanya kazi kubwa lakini hawakuwa na vitendea kazi, lakini kwa sasa tumefanya maboresho makubwa, na maboresho haya lazima yaendane na nyie kuwa na nidhamu kubwa,” alieleza Mej. Jen. (Mstaafu) Semfuko.
Kwa upande wake Prof. Suzana Augustino, Mjumbe wa Bodi hiyo, alisisitiza kuhusu matumizi ya teknolojia katika utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka hiyo hasa shughuli za uhifadhi ikiwemo ujangili na wanyama vamizi.
Prof. Suzana alisema teknolojia itarahisisha shughuli za uhifadhi kwenda kwa haraka na kwa wakati, kwani dunia kwa sasa imebadilika na ipo katika kipindi cha sayansi na teknolojia.
Kaimu Naibu Kamishna wa uhifadhi (TAWA) Mlage Kabange, ambaye alimuwakilisha Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA Mabula Misungwi Nyanda, alisema Mapori ya akiba manne yaliyopo chini ya Mamalaka hiyo katika Kanda ya Ziwa, yamekuwa na mchango mkubwa katika pato la Taifa.
Alisema Mapori hayo yamekuwa na shughuli mbalimbali za utalii wa picha, na utalii wa uwindaji, ambapo mchango wake kwenye mapato ya Mamlaka ni takribani asilimia 25.
“ Haya Mapori ya Akiba manne yaliyopo Kanda ya Ziwa, ni kati ya Mapori ya kimkakati ya Mamlaka. Yamekuwa na mchango mkubwa kwenye pato la Taifa, na tunaendelea kuboresha mazingira ya utekelezaji wa shughuli za uhifadhi kwenye mapori haya,” alisema Kabange.
Awali akisoma taarifa ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Mamlaka hiyo, Kaimu Kamanda wa Uhifadhi (TAWA) wa Kanda ya Ziwa Said Kabanda alisema katika kupambana na ujangili katika kipindi cha kuanzia Julai 2021 hadi Desemba 2023 jumla ya mitego ya nyaya 4,088 ilikamatwa kupitia doria 97,565 zilizofanywa na askari wa Mamlaka hiyo kwenye mapori hayo.
Aliongeza kuwa katika kipindi hicho jumla ya majangili waliokamatwa walikuwa 1,120 na kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufikishwa mahakamani.