Na Albano Midelo,Songea KUELEKEA kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani,Machi nane,wanawake Tawi la Boma Kuu Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma wamewafariji wafungwa na mahabusu wa Gereza la Mkoa kwa kutoa msaada wa vitu na vyakula mbalimbali.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi vifaa hivyo kwa Mkuu wa Gereza hilo ,Mwenyekiti wa Wanawake Tawi la Boma Kuu,Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Amina Tindwa amesema wanawake wa tawi hilo wamekabidhi vyakula na vifaa mbalimbali vyenye thamani ya shilingi 575,000.
Amevitaja vitu vilivyokabidhiwa kuwa ni mchele,sukari,sabuni za mche,,dawa za meno, miswaki,nyembe,taulo za kike,mafuta ya kupaka, mafuta ya kupikia,kandambili na nyama ya ng’ombe.
“Kuelekea kilele cha siku ya wanawake Duniani,sisi wanawake wa Boma Kuu Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma,tumeamua kufanya matendo ya huruma na kuungana na ndugu zetu wafungwa na maabusu waliopo katika Gereza la Mkoa ili kuwafariji na kuwatia moyo wasikate tamaa kwa kuwa hayo ni mapito ipo siku watarejea na kuungana nasi kulijenga Taifa’’,alisisitiza Tindwa.
Amebainisha kuwa magereza ni kama shule ya kujifunza na kujirekebisha ili wasirudie kutenda makosa ambapo ametoa rai kwao wakimaliza kifungo wawe mabalozi wazuri kwa kuwaelimisha wananchi wengine ili kuishi katika maadili yanayofaa na kufuata sheria,kanuni na taratibu za nchi.
Kwa upande wake Mkuu wa Gereza hilo Robert Mabeja amewashukuru wanawake wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma kwa msaada huo kwa wafungwa na mahabusu ambapo amesema kitendo kilichofanywa na wanawake hao kimeleta faraja kubwa kwao ambapo pia ameishukuru serikali ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa maboresho ya miundombinu yaliyofanyika katika Gereza hilo kongwe nchini.
Kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani kila mwaka hufanyika Machi nane ambapo katika Mkoa wa Ruvuma maadhimisho hayo kimkoa yanafanyika wilayani Mbinga.
Kaulimbiu ya mwaka huu ni “Wekeza kwa wanawake,kurahakisha maendeleo ya Taifa na Ustawi wa Jamii”.
Kaulimbiu hii inalenga kuhamasisha jamii kuwekeza kwa wanawake ili kuleta usawa wa kijinsia Pamoja na kukumbushana umuhimu wa usawa wa kijinsia katika kuchochea ukuaji wa Uchumi,maendeleo jumuishi na ustawi wa jamii kwa maendeleo endelevu kwa wanawake