Katika kuelekea kilele cha Maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto la Jeshi la Polisi Nchini ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Mtandao wa Polisi Wanawake Tanzania (TPF – Net) Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Maria Nzuki March 06, 2024 amewaongoza Mtandao wa Polisi Wanawake (TPF – Net) Makao Makuu ya Polisi Dodoma katika kutoa msaada kwa watoto njiti na watoto wenye uhitaji maalum katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
Akikabidhi msaada huo wa vitu vyenye thamani ya Tsh 1,495,000, DCP Nzuki alisema kuwa Mtandao wa Polisi Wanawake Makao Makuu ya Polisi wameona umuhimu wa kupeleka zawadi kwa Watoto wenye uhitaji maalum na Watoto njiti ikiwa ni kuunga mkono jitihada za Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ya kusogeza huduma bora kwa wananchi hasa katika maeneo ambayo huduma hiyo haipo.
Aidha, amewataka wananchi ambao kwa sasa ni wazima kiafya kushirikiana ili kuhakikisha kuwa wagonjwa ambao wapo hospitali wanapata mahitaji yanayohitajika ili afya zao ziweze kuimarika.
Kwa upande wake Muuguzi Mfawidhi wa Hopitali ya Rufaa ya Dodoma Stanley Mahundo, amewashukuru Mtandao wa Polisi Wanawake Makao Makuu ya Polisi kwa kuona umuhimu na kutambua uhitaji wa Watoto hao na kuamua kusambaza upendo kwa kutoa msaada huo ili kuwasaidia Watoto hao.
Naye Afisa Ustawi wa Jamii Hospitali ya Rufaa ya Dodoma Tegemea Ngurwa akipokea msaada huo, amewashukuru Wanamtandao huo wa Polisi kwa zawadi walizozitoa kwa ajili ya watoto hao na kusema kuwa msaada huo umekuja katika wakati sahihi.
Mtandao wa Polisi Wanawake Makao Makuu ya Polisi Dodoma limewasihi wananchi, taasisi na wadau mbalimbali kuendelea kujitokeza kutoa misaada ili kuwasaidia watoto hao njiti, watoto wenye uhitaji maalum pamoja na wagonjwa wengine.