Na: Dk. Reubeni Lumbagala, Kongwa, Dodoma.
Suala la utii wa sheria ni jukumu la kila mtu. Ni takwa la kisheria kwa kila mwananchi kuheshimu sheria za nchi katika nyanja zote kijamii, kiuchumi na kisiasa. Uvunjaji wa sheria na kujichukulia sheria mkononi ni kosa linalostahili adhabu kali. Mahakama ni mhimili ulio na jukumu la kuhakikisha haki inatendeka na pale sheria zinapovunjwa, mahakama inatoa adhabu dhidi ya mvunja sheria. Ipo lugha ya kisheria isemayo “Mtu yeyote hana hatia hadi pale atakapotiwa hatiani” (Everyone is innocent until proven guilty). Na ni mahakama ndiyo iliyopewa nguvu ya kisheria kumtangaza mtu kuwa ana hatia baada ya kufanyika michakato yote ya kisheria na hatimaye kuthibitika kuwa ana hatia kwa kuvunja sheria za nchi.
Mara kadhaa serikali kwa kushirikiana na asasi za kiraia pamoja na taasisi nyingine zisizo za kiserikali (NGOs) wamekuwa wakitoa elimu juu ya kuheshimu sheria kwa kuacha kujichukulia sheria mkononi hasa pale mtuhumiwa anapokuwa kwenye mikono ya wanajamii. Mathalani, mtu ameiba simu, jamii inapaswa kumkamata mtu huyo na kumfikisha katika kituo cha polisi ili kuacha sheria kuchukua mkondo wake badala ya kuanza kumpiga hadi wakati mwingine kufikia hatua ya kupoteza maisha akiwa kwenye mikono ya wanajamii. Hili halikubaliki hata kidogo.
Februari 27, 2024 katika kijiji cha Msambiazi wilayani Korogwe mkoani Tanga, kulitokea tulio la kusikitisha ambapo madereva wa pikipiki (bodaboda) wanatuhumiwa kulichoma moto basi la kampuni ya Saibaba Express baada ya dereva wa basi hilo kumgonga dereva wa bodaboda ambaye alifariki dunia. Baada ya kutokea tukio la dereva wa basi kumgonga dereva wa bodaboda, wananchi hao walipaswa kuuchukua mwili wa aliyegongwa na kuupeleka hospitali huku taratibu nyingine za kisheria dhidi ya dereva huyo zikifuata, lakini cha kushangaza na kusikitisha, watuhumiwa hao waliamua kulichoma basi moto, jambo ambalo ni kinyume kabisa na sheria za nchi.
Kufuatilia tukio hilo, Msemaji wa Jeshi la Polisi, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, David Misime alisema “Kitendo cha kuchoma basi kimedhulumu haki za watu wengine ambao hawakuhusika na tukio hilo la ajali, kwani mali za abiria ziliteketea kwa moto na kuwaingiza katika hasara kubwa na pengine kuwarudisha kwenye umaskini.” Basi hilo la Saibaba lilikuwa likifanya safari zake kati ya Dar es Salaam na Arusha, hivyo abiria waliokuwa wakisafiri walikuwa na majukumu mbalimbali ya kijamii na ya ujenzi wa uchumi wa nchi. Kuchomwa kwa basi walilokuwa wakisafiri nalo kumewaathiri kwani safari yao iliingia dosari kupitia tukio la uchomaji wa basi hilo. Kuteketea kwa mali za abiria ni kuwatia hasara isiyo na sababu na hivyo kuwarudisha nyuma kimaendeleo.
Katika taarifa ya habari iliyokuwa ikionyesha tukio hilo, kondakta wa basi hilo anasema wachomaji wa basi hilo walikuwa wakimuulizia kondakta wa basi yuko wapi ili waweze kumuua lakini aliwakimbia watu hao, hii ina maana kuwa wachomaji wa basi hawakuridhika na kuchoma basi moto lakini pia walitaka kumuua kondakta wa basi hilo. Ukatili huu si wa kuufumbia macho hata kidogo, ni muhimu hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya wote walioshiriki kitendo hiki cha kuchoma basi moto.
Msemaji wa Jeshi la Polisi aliendelea kusisitiza kuwa “Kuchomwa kwa basi hilo kumemwingiza mmiliki kwenye hasara ambayo si sahihi, kwani kilichotakiwa ni kusubiri vyombo vinavyosimamia sheria vichukue hatua dhidi ya dereva kwa mujibu wa sheria na si vinginevyo.” Wahusika wa uchomaji moto basi la Saibaba walipaswa kufikiri kwa makini kabla ya kuchukua uamuzi huo, kwani kuchoma basi moto hakuwezi kurejesha uhai wa dereva wa bodaboda aliyegongwa na hatimaye kufariki. Na pia walipaswa kufikiri kwa kina juu ya hasara kubwa atakayoingia mmiliki wa basi hilo kufuatia kuteketeza basi lake.
Pia, wachomaji wa basi walipaswa kuelewa mnyororo wa thamani uliopo kwenye basi hilo. Mathalani ajira kwa dereva na kondakta. Pia, kodi inayolipwa serikalini kupitia safari mbalimbali zinazofanywa na basi hilo na mwendelezo wa uwekezaji unaoweza kufanyika kupitia mapato yanayopatikana kupitia basi hilo. Lakini hayo yote wachomaji hawakufikiria na hatimaye kuteketeza basi hilo ambalo ni hasara kubwa kwa mmiliki na serikali kwani serikali itakosa mapato kupitia basi hilo.
Ni vyema jamii tukabadilika na kuepuka kujichukulia sheria mkononi kwani wahenga walisema “hasira hasara”. Zipo mamlaka zinazowajibika kuwaadhibu wavunja sheria za nchi, ni vyema mamlaka hizo zikaachwa zifanye kazi zake badala ya kuziingilia, jambo ambalo ni kinyume cha sheria. Nilipongeze Jeshi la Polisi kupitia Msemaji wake aliyesisitiza kuwa “Waliotekeleza tukio hilo wanasakwa na lazima wakamatwe kwa kuwa ni kinyume na sheria za nchi na ustawi wa amani.” Muhimu elimu juu ya utii wa sheria iendelee kutolewa kwa wananchi ili kumaliza tatizo la wananchi kujichukulia sheria mkononi na hatimaye kuepusha hasara zinazosababishwa na kujichukulia sheria mkononi ili kutorudisha nyuma juhudi zinazofanywa na serikali na watu binafsi za kukuza maendeleo yao na ya nchi pia. Tafakari, chukua hatua.
Dk. Reubeni Lumbagala ni Mwalimu wa Shule ya Mlali Sekondari iliyoko wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma. Maoni: 0620 800 462.