Mkurugenzi Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT),James Mbalwe akizungumza katika kikao kazi kati ya Bodi hiyo na Ofisi ya Msajili wa Hazina na Jukwaa la Wahariri Tanzania TEF kilichofanyika Chuo cha Utalii Posta Dar es Salaam Machi 6, 2024.
…………………..
Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT),katika kipindi cha mwaka 2022/2023 imechangia zaidi ya Sh bilioni 170 katika pato la Taifa ilizotokana na kodi.
Akizungumza jijini Dar es salaam leo March 06, 2024 katika kikao kazi baina ya jukwaa la Wahariri(TEF) na Bodi hiyo uliondaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina ikiwa ni mwendelezo wa taasisi na Mashirika yaliyo chini ya ofisi hiyo kueleza shughuli mbalimbali wanazozifanya Mkurugenzi Mkuu wa Bodi hiyo, James Mbalwe amesema kiasi hicho ni wastani wa ongezeko la asilimia 407 kwa mwaka katika kipindi hicho.
“Kodi imeongezeka sana kutoka Sh33.6 bilioni mwaka 2016/2017 ni matumaini yetu mpaka kufikia mwisho wa mwaka huu 2024 tutafikia Sh200 bilioni.
Amesema michezo ya kupahatisha inasisimua sekta ya michezo, uchumi na ukuaji wa utalii kutoka na baadhi ya wageni kucheza kwa kutumia fedha za kigeni.
Amesema wamekuwa na Jukumu la kuishauri serikali kuhusu ukusanyaji wa kodi amapo wao ndio washauri wakuu wa kodi zote za michezo ya kubahatisha kama serikali inataka kufanya maboresho lazima wao ndio waishauri na hii ni kwa mujibu wa sheria.
Amesema Zipo kodi ambazo walizianzishia utaratibu ambazo zinakuwa zinalipwa kwa wiki hakuna sekta yoyote inayolipa hivyo kwa wiki isipokuwa michezo ya kubahatisha huu ndio upekee wa sekta hii.
Hata hivyo amesema kuwa wanafanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kubaini waendeshaji wapya walioingia kama bado wanasifa ambazo waliingia nazo na kupewa leseni.
“Tukiona wakati wowote umetoka kwenye vigezo na sifa tulizokuwekea tunachukua leseni yetu na ndio maana tunafanya uchaguzi wa kugundua maeneo gani ni sahii na yapi sio sahihi”,Amesema.
Aidha ameongeza kuwa pamoja na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara bado kunachangamoto kubwa ya waendeshaji wa michezo hiyo kihalamu yaani pasipo leseni.
Sambamba na hayo amesema pamoja na uzuri wa sekta hiyo wanajitahidi kutoa elimu ili mchezo huo usije kuwa na madhara kwa jamii kwani sekta hiyo isiposimamiwa vizuri inaweza ikaleta madhara.
Aidha Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa jamii inapaswa kushirikiana katika kupiga vita vitendo visivyokubalika kama kuwahusisha watoto wadogo chini ya miaka 18 kushiriki katika michezo hiyo.
Amesema pia wametunga sheria ya kumlinda mtoto kwani hawaruhusiwi kujihusisha na michezo hiyo na yeyote atakaekutwa anamchezesha mtoto hatua kali za kisheria zinachukuliwa ikiwa ni pamoja na kumnyang’anya leseni na kupelekwa mahakamani.
Ameongeza kuwa michezo ya kubahatisha ipo ya aina mbili ambapo moja ya kibiashara ambayo wanalipa kodi na mingine ni kwa ajili ya kukuza biashara ama kusaidia jamii ikiwemo uendeshaji wa majumba ya Casino.
Hata hivyo, Mkurugenzi huyo amesisitiza kuwa Michezo ya kubahatisha si ajira bali ni Burudani wala siyo chanzo cha mapato.