Mamlaka za Maji zimetakiwa kuwa na nyenzo muhimu katika utendaji kazi ili kukabiliana na upungufu wa aina yoyote utakaojitokeza katika kufikisha huduma ya maji kwa jamii.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Mwajuma Waziri ametoa agizo hilo jijini Mwanza akifungua Mafunzo ya Uandaaji wa Maandiko ya Miradi ya Maji kwa Mamlaka za maji nchini.
Amewataka washiriki wote kutumia vyema fursa ya mafunzo hayo ili kuboresha makusanyo ya fedha katika maeneo yao ya kazi na kuwa na njia mbadala katika usimamizi na uendelezaji wa miradi ya maji hapa nchini.
Mhandisi Mwajuma amesema atafanya ufuatiliaji wa karibu hususani kwa mamlaka zote zilizoshiriki mafunzo hayo Ili kuweza kupata mrejesho kuhusu utekelezaji wa yaliyotokana na mafunzo.
Kupitia mafunzo hayo mamlaka za maji zitaweza kuandaa maandiko bora yatakayo wezesha upatikanaji wa fedha kwa taasisi zinazo toa mikopo ikiwemo Mfuko wa Taifa wa Maji katika kufanikisha jukumu la kufikisha huduma ya maji katika jamii.