Na: Dk. Reubeni Lumbagala, Kongwa-Dodoma.
NIANZE makala haya kuungana na watanzania wenzangu kutoa pole kwa serikali, familia, ndugu, jamaa na marafiki kufuatia kifo cha Rais Mstaafu wa awamu ya pili Hayati Ali Hassan Mwinyi (98) kilichotokea Februari 29, 2024. Taarifa ya kifo ilitolewa na Rais Samia Suluhu Hassan ambapo alisema “Kwa majonzi makubwa nasikitika kutangaza kifo cha Rais Mstaafu wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi, aliyefariki dunia leo Februari 29 saa 11 jioni katika Hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu ya saratani ya mapafu. Mzee Ali Hassan Mwinyi amekuwa akipatiwa matibabu tangu Novemba mwaka jana huko London, Uingereza na baadaye kurejea nchini na kuendelea na matibabu katika Hospitali ya Mzena”. Machi 2, 2024, Hayati Ali Hassan Mwinyi alizikwa rasmi kijijini kwake Mangapwani Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Hayati Ali Hassani Mwinyi alipokea kijiti ya Urais kutoka kwa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, na hii ikamfanya kuingia kwenye rekodi ya kuwa Rais wa awamu ya pili. Hayati Ali Hassani Mwinyi ni hazina kubwa kwa taifa letu kutokana na mambo mengi mazuri aliyoyafanya enzi za utumishi wake alishika nyadhifa mbalimbali na baadaye kushika nyadhifa ya juu kabisa ya nchi yani Rais.
Makala haya yanaangazia juhudi kubwa alizofanya katika kuinua uchumi wa nchi kwani wakati alipoingia madarakani, hali ya uchumi ilikuwa ni mbaya ambapo kulihitajika mikakati madhubuti ya kuweza kuinua uchumi wa nchi. Kazi kubwa aliyoifanya Hayati Mwinyi inampa sifa ya kuitwa “Baba wa Mageuzi ya Kiuchumi.”
Ikumbukwe kuwa moja ya jukumu kubwa la serikali ni kuwahudumia wananchi kwa kuhakikisha inaweka mikakati, mipango na mazingira wezeshi ya kiunua maendeleo ya mtu mmoja mmoja na maendeleo ya nchi kwa ujumla. Aidha, suala la maendeleo yawe ni ya kisiasa, kijamii au kiuchumi si suala lelemama, ni kazi nzito yenye kuhitaji kuunganisha nguvu ya pamoja ili kufanikiwa azma hiyo.
Hayati Mwinyi baada ya kuchaguliwa kuwa rais mwaka 1985 aliikuta nchi katika mazingira magumu ya kiuchumi. Changamoto za wakati huo alizokumbana nazo ni pamoja na athari za vita ya Tanzania na Uganda mwaka 1978-1979, kupanda bei ya mafuta, ukame na masharti magumu ya wahisani. Kutokana na changamoto hizi, Hayati Mwinyi alilazimika kufanya mabadiliko ya kisera na kisiasa ili kuchochea ukuaji wa uchumi na hatimaye kufikia azma ya serikali yake ya kukuza maendeleo ya nchi.
Hayati Mwinyi akawa mwasisi wa sera ya ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (Public and Private Partinership – PPP). Katika kipindi cha uongozi wake, alitoa fursa ya ushiriki wa sekta binafsi katika ujenzi wa uchumi wa nchi ambapo hii ilikuwa ni fursa adhimu ya kuongeza wigo wa ushiriki wa wananchi katika ujenzi wa uchumi.
Msisitizo wa soko huria (free market) ulipewa msukumo wa kipekee katika kipindi cha uongozi wake ambapo sekta binafsi ilipewa uhuru wa kufanya biashara badala ya jukumu hilo kubaki kwa serikali chini ya mfumo wa ujamaa. Moja ya sababu iliyochangia Hayati Mwinyi kupewa jina la “Mzee wa Ruksa” ni uamuzi wake wa kutoa ruhusa na fursa kwa watu binafsi kushiriki katika ujenzi wa uchumi wa nchi, jambo ambalo kwa miaka mingi haikufanyika na hivyo jukumu hilo kubaki kwa serikali pekee.
Kutokana na ugumu uliopo wa ujenzi wa nchi, ni muhimu sekta binafsi kushirikishwa moja kwa moja katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na uwekezaji ili kurahisisha kasi ya maendeleo. Hivyo basi, uwekezaji binafsi ulioruhusiwa enzi za uongozi wa Hayati Mwinyi ulisaidia kuinua uchumi na kupunguza makali ya maisha kama vile uhaba wa chakula, nguo na mafuta. Akimzungumzia Hayati Mwinyi, Mwanasiasa mkongwe nchini Dk. Wilbrod Peter Slaa amesema “Mzee Mwinyi alipokuja na sera yake ya kufungua madirisha na milango, basi kila upepo uliingia vizuri na tukapata nafuu tofauti na ilivyokuwa kabla, ambapo hata dawa ya meno ilikuwa ngumu kuipata. Kiukweli, aliingia kipindi kigumu, akafanya kazi na Watanzania hawatamsahau kwa hilo na ndiyo maana wanamuita mzee ruksa.”
Ni ukweli kuwa ili kuongeza kasi ya maendeleo, ni lazima serikali iwe na fedha za kutosha za kuibua na kutekeleza miradi ya maendeleo na ile ya kimkakati. Kutokana na ugumu wa serikali kufanya kila kitu pekee yake, ndipo umuhimu wa ushirikishaji wa sekta binafsi inapoonekana. Na ndiyo maana Hayati Mwinyi aliishirikisha kikamilifu sekta binafsi ambayo ilichangia ongezeko la makusanyo ya mapato na hivyo kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi na hatimaye kufikia maendeleo ya kweli ya nchi. Ni katika kipindi chake cha uongozi ambapo uhuru wa vyombo vya habari ulitamalaki. Vyombo vya habari vinaitwa muhimili wa wanne usio rasmi kutokana na umuhimu wake katika kuchagiza maendeleo.
Watu binafsi waliruhusiwa kumiliki vyombo vya habari. Mathalani Hayati Mwinyi alimpongeza marehemu Reginald Mengi kwa kuanzisha vyombo vya habari kama vile ITV, Radio One, magazeti ya Nipashe na The Guardian. Uhuru wa vyombo vya habari umekuwa chachu ya kuharakisha maendeleo kutokana na kuibua changamoto mbalimbali ambazo imeilazimu serikali kufanyia kazi na hivyo kuchochea kasi ya maendeleo nchini.
Msukumo wa ushirikishwaji wa sekta binafsi kwenye uchumi umeendelea kuenziwa kwa vitendo na marais wote waliofuata baada yake yaani serikali ya awamu ya tatu hadi hii ya sita ya sasa. Hii imesaidia kuipunguzia serikali mzigo wa kuwahudumiwa wananchi wake na hivyo huduma muhimu za kijamii kuwafikia wananchi kule walipo. Hakika Hayati Ali Hassan Mwinyi utakumbukwa daima kwa kuweka misingi bora ya uchumi hasa ushirikishwaji wa sekta binafsi katika maendeleo ya nchi.
Dk. Reubeni Lumbagala ni Mwalimu wa Shule ya Mlali Sekondari iliyoko wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma. Maoni: 0620 800 462.