Na Timoth Anderson
Zaidi ya wataalamu 450 wa elimu bila ukomo toka Tanzania Bara na Zanzibar wamekutana jijini Dar es salaam kwenye kongamano la kitaifa kuhusu elimu bila ukomo kwa lengo la kujadili kuhusu nafasi ya elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi pamoja na mustakabadhi wake kwa maendeleo ya jamii na Taifa.
Kongamano hilo lililoandaliwa na Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) limezinduliwa tarehe 1 Machi, 2024 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyn Nombo aliyemwakilisha Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda.
Prof. Nombo amesema Serikali ya Awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imedhamiria kwa dhati katika kuhakikisha maboresho ya Sera ya Elimu na Mafunzo 2014, pamoja na mitaala yanagusa mifumo yote ya utoaji elimu na si mfumo rasmi pekee.
Mabadiliko yanatakiwa katika sekta ya elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi vilevile kukuza fursa za elimu isiyo na ukomo kwa watu wote na kumjenga mtanzania mwenye utamaduni wa kupenda kujisomea na kujiendeleza katika muktadha wa elimu bila ukomo. amesema
Mkurugenzi wa Elimu Msingi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Ndugu Abdul Maulid amesema elimu bila ukomo kwa karne ya sasa, sio kusoma, kuandika wala kuhesabu bali inaelekeza kuwepo kwa mifumo ya ujifunzaji endelevu na nyumbufu, ikijumuisha sehemu tatu muhimu yaani mfumo rasmi wa elimu; elimu nje ya mfumo rasmi; na elimu ya watu wazima.
Elimu bila ukomo ni muhimu kwa sababu ya mabadiliko yanayoendelea kutokea kila wakatiSuala hili ni muhimu sana kwa kuwa linahusisha pia uwezo wa kumudu stadi za karne ya 21 ambazo ni stadi za kisomo,stadi za ujifunzaji,na stadi za maisha. amesisitiza.
Kwa upande wake Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima Prof. Michael Ngumbi ameeleza kwamba TEWW inatekeleza elimu bila ukomo ambapo imeandaa kongamano hilo ambalo litawezesha Taasisi hiyo kutoa elimu kwa namna bora kutokana na matakwa ya mahitaji ya sasa.
Kongamano hilo imejadili kuhusu maboresho ya sera na mafunzo kwa kujadili nafasi ya elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi, mtazamo wa kisheria kuhusu elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi, ushirikishwaji wa wadau katika utekelezaji wa elimu bila ukomo, uzoefu wa elimu bila ukomo kutoka nchi nyingine pamoja na utekelezaji wa elimu bila ukomo katika muktadha wa sera mpya ya elimu.
Washiriki wa kongamano hilo wametoka kwenye Taasisi mbalimbali za Serikalini, mashirika ya kimataifa na wadau wa maendeleo ya sekta ya elimu.