Na. Zainab Ally Mikumi.
Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imeendesha mafunzo ya Usalama wa Anga kwa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kwa lengo la kudhibiti vihatarishi mbalimbali vinavyoweza kujitokeza katika viwanja vya ndege vinavyopatikana ndani ya shirika hilo, mafunzo yatakayochukua siku 5 kuanzia leo Machi 04, 2024 hadi Machi 08, 2024.
Akitoa mafunzo hayo Mkufunzi Mkuu wa Chuo cha Usafiri wa Anga Tanzania (CATC) Thamarat Abeid alisema, “Lengo la mafunzo hayo ni kutoa elimu inayohusiana na usalama wa viwanja vya ndege ili kujua sheria, kanuni na taratibu za Shirika mama la Usafiri wa Anga duniani – ICAO pamoja na kanuni na taratibu ambazo zimetolewa na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania – TCAA ili wataalam wetu hawa wafanye kazi kwa ufasaha na kuleta tija kwa taifa na dunia kwa ujumla”.
Aidha, mkufunzi huyo aliongeza kuwa mafunzo haya yatahusisha vihatarishi mbalimbali vilivyopo katika viwanja vya ndege, utoaji wa taarifa ambazo ni muhimu sana ili wamiliki wa ndege na marubani wapate wigo mpana wa uelewa hata kama itatokea changamoto ijadiliwe kwa pamoja na kupata muafaka wa pamoja kati ya wamiliki wa viwanja, marubani, wamiliki wa ndege na Mamlaka ya Usafiri wa Anga.
Naye, Afisa Uhifadhi Mkuu anayesimamia viwanja vya ndege TANAPA Christine Bgoya alisema, kwenye mafunzo haya tunao Maafisa na Askari kutoka Idara za Utalii na Miundombinu ambao wanahusika moja kwa moja na masuala haya ya viwanja vyetu vya ndege, hivyo kuwepo kwao hapa kutawaongezea uelewa wa kuviendesha viwanja hivi kitaalam zaidi tofauti na ilivyokuwa awali.
Pia, Mhifadhi Bgoya aliongeza, “Lengo la kuomba mafunzo haya kutoka kwa wenzetu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga ni kutokana na ongezeko kubwa la idadi ya watalii wanaotumia usafiri wa anga, mathalan kwa takwimu za mwaka huu kwa Hifadhi ya Taifa Mikumi zaidi ya nusu ya watalii wote wa nje hutumia ndege, hivyo ni wakati muafaka kwa TANAPA kupata mafunzo haya.”
Vilevile, Kamishna Msaidizi Fredrick Malisa akimwakilisha Kamanda Uhifadhi Kanda ya Mashariki, aliwashukuru wakufunzi hao kwa mafunzo hayo na kuwadokeza kuwa usafiri wa anga kwa upande wa TANAPA ni nguzo muhimu sana katika mnyororo wa kukuza utalii nchini.
Aidha, Kamishna Malisa alisema, “Shirika linatambua kwamba ili kazi za usalama wa viwanja vya ndege zifanyike kwa ufanisi ni lazima watumishi wanaofanya kazi hizo kujengewa uwezo, na ndio maana leo tuko hapa tukipewa mafunzo ya kibobezi na wataalam wetu kutoka Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania. Hivyo tuwahakikishie hayo yote mnayotufundisha tutayafanyia kazi.”
Mafunzo hayo ya usalama wa viwanja vya ndege yanafanyika kwa siku tano mfululizo kuanzia leo Machi 04, hadi 08, 2024 katika Hifadhi ya Taifa Mikumi iliyoko mkoani Morogoro.