CHANZO – BEST MEDIA
HALMASHAURI Kuu ya Chama ACT Taifa iliyokutana kwenye Ukumbi wa Hakainde Hichilema uliopo kwenye Jengo la Maalim Seif Makao Makuu ya Chama hicho, imeridhia uamuzi wa Ndugu Juma Duni Haji kujitoa kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Chama Taifa wa ACT Wazalendo.
Taarifa iliyotolewa leo Machi 4, 2024 ikiwa siku moja kabla ya kuanza kwa vikao vya uchaguzi Mkuu wa chama hicho, na Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu, ilieleza kuwa kwenye hotuba yake kwa Halmashauri Kuu, uma Duni, Mwenyekiti wa Chama Taifa ameeleza kuwa “Leo tarehe 4/3/2024 mchana huu nimekabidhi rasmi barua yangu kwa Katibu wa Kamati Maalum ya Uchaguzi Taifa na kuinakilisha barua hiyo kwa Katibu Mkuu wa Chama na Mwenyekiti wa Kamati Maalum ya Uchaguzi Taifa-kwa taarifa na hatua zao, kuhusu kuondoa nia (kujitoa) kugombea nafasi ya Uenyekiti wa Chama Taifa.
“Nimechukua uamuzi huo kwa mujibu wa Katiba ya Chama Ibara ya 11(3)(7) na Ibara ya 76(1)(p) na Ibara ya 111(3) zikisomwa pamoja, juu ya haki ya kuchagua na kuchaguliwa kuwa Kiongozi, kazi na wajibu wa Halmashauri Kuu ya Chama kuwa ni “kujadili na kuidhinishwa na majina ya wagombea wa nafasi za Kiongozi wa Chama, Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Chama”.
“Hivyo napenda kuchukua fursa hii kuwaomba viongozi wenzangu na Wajumbe wa Halmashauri Kuu kuridhia kujitoa kwangu katika mchakato wa kugombea nafasi hiyo na kutopoteza muda wenu kutekeleza takwa la Katiba Ibara tajwa hapo juu,” amesema Duni katika hotuba yake
Akizungumza kuhusu sababu za kuondoa jina lake, Mwenyekiti wa Chama, Juma Duni Haji amesema
Amesema amefikia uamuzi huo kwa kuzingatia sabau zifuatazo, ikiwamo kuzingatia maslahi mapana ya Taasisi yetu, kuzingatia ushauri, maoni na au mapendekezo ya viongozi wenzake.
“Kuondoa taharuki iliyojitokeza, kuimarisha umoja na maelewano miongoni mwetu, kuelekeza nguvu zote sote dhidi ya washindani wetu wa kisiasa na kutotoa nafasi ya mgawanyiko miongoni mwetu
“Kumuachia Ndugu Othman Masoud Othman akabidhiwe nafasi hii aendeleze mapambano ya kudai haki. Nimetekeleza haki ya kikatiba,” amesema
Pamoja hiyo amesema kuwa “Mimi Ndugu Juma Duni Haji nimejiunga katika harakati za kudai haki na ukombozi kwa nchi zetu miaka 30 iliyopita ndani ya mfumo wa Vyama vingi vya siasa nikiamini kuwa kufanya hivyo nitatoa mchango wangu katika kuwaunganisha Watanzania ili wakatae uonevu, kudhalilishwa, kunyanyaswa, kubaguliwa au maovu mengine yanayoweza kufanywa dhidi ya heshima ya utu wa binadamu, yawe yanayotendwa na serikali, kikundi cha watu walio na uwezo, kwa ajili ya matakwa yao, au kwa ajili ya kujinufaisha kwao kiuchumi, au kisiasa na au kiitikadi, au kwa ajili ya dini, kabila, jinsia au rangi zao..na nitaendelea na msimamo huo. Mapambano ya kudai haki lazima yaendelee,” amesema