Meneja wa Tanroads mkoa wa Ruvuma Mhandisi Saleh Juma kulia na wasaidizi wake  Roman Mbukwin  kushoto,mwakilishi wa kampuni ya Ovans Contruction Ltd Azimio Mwapongo na  Godfrey Robbi wa pili kulia,wakikagua eneo la barabara lililoharibika na mvua zinazoendelea kunyesha kwa wingi wilayani Tunduru.

 Mhandisi Azimio Mwapongo kutoka kampuni ya Ovans Contruction Ltd aliyenyoosha mkono,akiwaonyesha kina cha maji katika mto Muhuwesi wilayani Tunduru wahandishi kutoka ofisi ya Tanroads mkoa wa Ruvuma ambao  maji yake yanakuwa yanapita juu ya daraja la Muhuwesi na kusababisha adha kubwa kwa watumiaji wake.

Meneja wa Tanroads mkoa wa Ruvuma Mhandisi Saleh Juma kushoto,akizungumza na wahandisi kutoka ofisi ya Tanroads mkoa Mhandisi Godfrey Robbi kulia na Roman Mbukwin wa pili kulia na mhandisi kutoka kampuni ya Ovans Contruction Ltd Azimio Mwapongo wa pili kushoto, baada ya kukagua miundombinu ya barabara ya Tunduru-Mangaka  iliyoharibiwa na mvua za masika zinazoendelea kunyesha kwa wingi  mkoani humo.
…………….

Na Mwandishi wetu
Tunduru

WAKALA wa Barabara nchini(Tanroads)mkoa wa Ruvuma,imewatoa hofu watumiaji wa barabara kuu ya Songea-Mangaka kwamba daraja la mto Muhuwesi wilayani Tunduru ambalo lilipata athari ya moja ya sehemu yake kusogea pembeni kwa sasa liko salama.

Hayo yamesemwa jana na meneja wa Tanroads mkoani hapa Mhandisi Saleh Juma, baada ya kukagua kazi ya marekebisho ya daraja hilo  linalounganisha mkoa wa Ruvuma na mikoa jirani ya Lindi,Mtwara Pwani na Dar es slaam.

Alisema,Tanroads kwa kumtumia mkandarasi imefanya kazi ya kurudisha sehemu ya kipande kilichotoka sehemu yake na hata maji yalivyopita juu kwa mara ya pili hayakuathiri  miundombinu ya daraja hilo muhimu kwa uchumi wa mikoa ya kusini na nchi kwa ujumla.

Salehe alisema,iwapo itatokea tena daraja hilo kufunikwa na maji watumiaji watalazimika kusubiri hadi yatakapopungua kwa ajili ya usalama wao ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea.

Aidha alieleza kuwa,wamemtafuta mhandisi mshauri ambaye atashauri namna bora ya  kuboresha daraja hilo ili liendane na kiwango cha maji kinachopita katika mto Muhuwesi kama daraja hilo lipandishwe juu au  lijengwe lingine.

Msimamizi wa kitengo cha matengenezo Tanroads mkoa wa Ruvuma mhandisi Roman Mbukwini alisema,kwa sasa  kazi inayofanyika ni kuimarisha baadhi ya sehemu ya barabara ambazo zimeathirika na maji kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha kwa wingi wilayani humo.

Alisema,mvua  hizo zimesababisha baadhi ya maeneo ya barabara maji kupita chini ya ardhi na kuharibu miundombinu,lakini tayari serikali kupitia Tanroads inafanya marekebisho ili kurahisisha shughuli ya usafiri na usafirishaji.

Mkazi wa Tunduru  Daniel Peter,ameshauri daraja hilo lipandishwe juu na mto Muhuwesi upanuliwe ili maji yasipite juu ya daraja kwa usalama  wa wananchi na miundombinu ya daraja.

Alisema,changamoto kubwa katika daraja hilo ni maji ya mvua kupita juu hivyo kusababisha adha kubwa kwa watumiaji ambao wanalazimika kusubiri kati ya masaa matatu na manne ili maji yapungue na waweze kuendelea na safari zao.