Ashrack Miraji, Same Kilimanjaro
Mbunge wa jimbo la Same Mashariki Mkoani kilimanjaro,Anne Kilango amewataka viongozi jimboni hapo kushirikiana kwa pamoja kusimamia miradi ya maendeleo ili kurahisisha utekelezaji wa majukumu yao.
Wito huo umetolewa kwa viongozi wa jumuiya ya wazazi (UWT),madiwani,makatibu tawala wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Same.
Mbuge Kilango ametoa maelezo hayo katika semina kati yake na baadhi ya viongozi hao kilichofanyika jijini Dodoma katika ukumbi wa Samwel Sitta.
Amewataka jumuiya zote za Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutekeleza ilani ya chama na kumsaidia Rais kutekeleza miradi inayotekelezwa jimboni hapo.
“Niwaombe viongozi wenzangu,Madiwani wa viti maalumu,wenyeviti na Makatibu wa UWT na jumuiya ya wazazi ngazi ya kata kuendelea kushirikiana kwa pamoja, lengo likiwa ni kuimarisha jumuiya zetu ziendelee kudumu na kusimamia miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika jimbo letu”
Pamoja na kuwataka wawe na ushirikiano baina yao wakiwa kazini,pia amezitaka jumuiya zote jimboni Same kumsemea vizuri kwa wananchi wake,Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dk Samia Suluhu Hassan kwa kusimamia vizuri miradi ya maendeleo.
“Hakikisheni mnamsaidia Rais kusimamia miradi inayotekelezwa jimboni au kata,hii siyo kazi ya Mbuge pekee yake bali kwa kushirikiana kwa pamoja huku lengo likiwa ni kujenga jimbo letu kwa pamoja na kuwasaidia wananchi kwenye nyanja mbalimbali za maendeleo,” alisema mbunge Kilango.
Aidha amesema jumuiya zote za Chama Cha Mapinduzi (CCM) zinatekeleza ilani ya chama hicho,hivyo zinapaswa kuwezesha mipango na mikakati mbalimbali ya serikali na amethibitisha kuwa anawaamini viongozi hao na anatarajia watafanya vizuri.
Katibu Mkuu Msaidizi Mwandamizi wa sehemu ya vikao na Mafunzo ya Chama,Idara ya Organization Taifa,Kajor Johoroka amempongeza mbunge Kilango kwa kuandaa semina hiyo ambayo amesema itakuwa chachu ya maendeleo kwa viongozi wa jimboni hapo.
“nampongeza Mhe. Mbuge Anne kilango kwa hiki kitendo alichokifanya kuandaa semina kwa wasaidizi wa jimboni kwake ambao mnafanya Kazi kubwa ya kumsaidia Mhe Rais Dk Samia Suluhu Hassani Katika kusimamia Miradi”
Vilevile ameziomba jumuiya zote kuwa kitu kimoja hasa Katika kuleta maendeleo na kuimarisha umoja wao na kutokuwepo Mtu wa kuwayumbisha katika kutekeleza ilani ya Chama cha Mapinduzi.